Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uteuzi imemuidhinisha wakili Dorcas Oduor kama mwanasheria Mkuu na Beatrice Askul Moe kama waziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki na masuala ya Kikanda.
Hii ilifuatia uhakiki wao uliofanyika mnamo Ijumaa, Agosti 9, 2024.
Ripoti ya kamati hiyo imewasilishwa katika Bunge la Kitaifa na kiongozi wa Wachache bungeni Junet Mohamed.
“Bunge hili limeidhinisha uteuzi wa watu wafuatao, Beatrice Askul Moe kama waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda na Dorcas Oduor kama Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Kenya,” alisema Junet.
Wawili hao sasa wanasubiri kuidhinishwa na kikao cha Bunge la Kitaifa kabla ya majina hayo kutumwa kwa Rais William Ruto kwa ajili ya kuchapishwa kwenye gazeti la serikali na baadaye kuapishwa.
Ikumbukwe kuwa wawili hao walikuwa katika kundi la mwisho la mawaziri walioteuliwa na Rais William Ruto.
Askul ni mwanasayansi wa masuala ya kijamii na awali alihudumu kama waziri wa Maji na Usafi wa Mazingira katika kaunti ya Turkana, na hadi kuteuliwa kwake alikuwa akihudumu kama mwanachama wa Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Uchaguzi wa chama cha ODM.
Naye Oduor, aliyeteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu (AG) hadi uteuzi wake alikuwa Katibu katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ODPP; atakapoidhinishwa na bunge zima na hata kuapishwa atakuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa kike nchini Kenya.
By Mjomba Rashid