Huenda Wakenya wakapata afueni kiasi cha haja ya changamoto za kiuchumi zinazowalemea nchini Serikali ikipanga kupunguza Ushuru wa Thamani kwa Bidhaa (VAT) na ushuru mwingine.
Hazina ya Kitaifa ya Fedha katika bajeti yake ya muda wa kati inakusudia kupunguza ushuru wa VAT kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14 pamoja na kupunguza ushuru wa shirika na ushuru mwingine.
Akizindua mchakato wa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2025/2026 mnamo Jumatatu Septemba 9, Waziri wa Fedha John Mbadi amesema katika kipindi hicho Wizara haiwazii kuongeza viwango vya ushuru bali kumpunguzia mwananchi mzigo wa gharama.
“Katika kipindi cha kati ya muhula tunataka kupunguza viwango vya ushuru, hatufikirii kuongeza ushuru. Tutapunguza ushuru wa VAT kutoka asilimia 16 hadi 14, na pia ushuru mweingine ule wa ushirika kutoka asilimia 30 hadi 20. Hivi ndivyo tunavyowaza kama Hazina, hatuwazii kuongeza ushuru kabisa.” Alisema.
Waziri Mbadi aidha amebaini kuwa Serikali haitaunga mkono matumizi yoyote ya ziada na badala yake itaangazia kuimarisha ufanisi, uwajibikaji na matumizi ya busara ya raslimali.
Waziri huyo amesema kuna mipango ya kutekeleza mfumo mpya wa kudhibiti fedha lengo hasa likiwa ni kushinikiza uwazi katika mchakato wa manunuzi ya serikali.
Wakati uo huo Mbadi amesema utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa Kifedha wa 2024/2025 umeanza kwa dhati.
BY MJOMBA RASHID