HabariNews

Waziri Chirchir Akataa Kutoa Stakabadhi za Makaubaliano ya Kuukabidhi Uwanja wa Ndege JKIA kwa Kampuni ya Adani

Utata unaozingira pendekezo la kuukodisha uwanja wa Kimataifa wa ndege wa JKIA kwa Kampuni ya India ya Adani umezidi kuongezeka huku Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir kushindwa kupeana stakabadhi muhimu mbele ya bunge la Seneti.

Huku akithibitisha kuwa kuna pendekezo la uwekezaji lililoanzishwa kibinafsi na kampuni ya Adani Group la kuendeleza, kuendesha na kuhamisha JKIA chini ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Waziri huyo hakutoa statakabdhi hizo.

Amesema atatoa stakabadhi na taarifa zaidi punde tu kamati itakapoamua kuhusu suala hilo, hatua iliyowaghadhabisha maseneta wanachama wa Kamati ya Seneti ya Barabara na Uchukuzi, waliomshtumu waziri huyo kuendelea kukwepa kutoa taarifa muhimu.

Ukosefu wa stakabadhi za mkataba huo umeibua tetesi na tumbojoto kutoka kwa maseneta hao ambao walikuwa wametaka ziwekwe wazi kabla ya kikao hicho kuendelea, huku Waziri Chirchir akisema kuwa angeziwasilisha baadaye.

Nalicha ya Maseneta kudai kulikuwa na makubaliano ya kimkataba kati ya Kampuni ya Adani na Serikali ya Kenya kuiwezesha kampuni hiyo kusambaza umeme kupitia kampuni ya KETRACO, kukabidhiwa Kampuni ya umeme ya KenGen n ahata pia kuendesha mpango mpya wa Bima ya Afya ya Jamii, SHIF.

Waziri Chirchir pia amedai kuwa hawezi kutoa taarifa mbele ya kamati hiyo kwa kuwa suala hilo lilikuwa tayari mahakamani na wizara yake ilikuwa imeapwa maagizo mawili ya mahakama kuhusu masuala hayo.

BY MJOMBA RASHID