Waziri wa Barabara na Uchukuzi Davis Chirchir amethibitisha kuwa Kampuni ya Adani kutoka India imewasilisha pendekezo kwa Kampuni ya kusambaza umeme ya KETRACO.
Katika ombi lake hilo iwapo litaidhinishwa Adani Group itamiliki na kuchukua usimamizi wa laini kadhaa za umeme nchini.
Chirchir ambaye awali alikuwa Waziri wa Kawi, amefichua kuwa kampuni hiyo ya Adani imeonyesha nia ya kutaka kuendesha laini ya umeme ya Gilgil-Thika-Malaa iliyoko chini ya KETRACO, japo pendekezo hilo halijakamilika kwani lingali linafanyiwa tathmini.
Ikumbukwe kuwa Seneta wa Kisii Richard Onyonka mnamo siku ya Alhamisi katika Kikao cha Kamati ya Seneti kuhusu Barabara na Uchukuzi, kilichohudhuriwa na Waziri huyo, ndiye aliyefichua kuwa kulikuwa na makubaliano kati ya Adani na KETRACO.
Haya yanajiri huku kampuni hiyo ya Adani ikishtumiwa pakubwa nchini kwa kuingia mkataba na serikali kukodishiwa na kuchukua uwanja wa Kimataifa wa ndege wa jkia kwa muda wa miaka 30, kuukarabati na kuendesha shughuli.
By Mjomba Rashid