HabariNews

Asilimia 95 ya waathiriwa wa visa vya unyanyasaji wa kingono mitandaoni ni wavulana

Asilimia kubwa ya visa vya unyanyasaji wa kingono wanavyofanyiwa wavulana mitandaoni hukosa kuripotiwa kwa hofu ya kukosa kuchukuliwa kwa hatua mwafaka katika kushughulikia visa hivyo kutoka kwa idara ya usalama.

Visa vya unyanyasaji wa kingono na ulanguzi wa watoto vikiendelea kuripotiwa imebainika kuwa wavulana wamekuwa na uzito wa kuripoti visa hivyo vinapowatokea, licha ya kubainika kuwa takriban asilimia 95 ya waathiriwa wa visa hivyo ni wavulana.

Akizungumza huko Diani kaunti ya Kwale, kwenye warsha iliyoandaliwa na shirika la kimataifa la kupigania haki za binadamu la IJM, kuhusu unyanyasaji na ugomvi wa kjinsia dhidi ya wanawake na watoto, Mueni Mutisya ofisa wa kusimamia maslahi ya watoto katika idara ya upelelezi DCI, anasema kupitia ushirikiano na wadau mbali mbali wamefanikiwa kupata taarifa za visa hivyo huku akieleza kuwa hakuna kesi yoyote iliyowahi kutupiliwa mbali kwa kukosa ushahidi wa kutosha.

“Asilimia kubwa ya kesi tunazokabiliana nazo ni za wavulana. Nyingi ya kesi hizi ni zile ambazo zimeripotiwa kupitia mpango wa NACMEC kwasababu wavulana wengi, na watoto pia hawapigi ripoti wanapofanyiwa visa kama hivi, kwakuwa wanaamini kuwa maafisa wa polisi hawawezi kuchukua hatua na kushughulikia kesi hizo. Kwanza naweza kusema tangu kitengo hiki kiasisiwe hakuna kesi hata moja ambayo imetupiliwa mbali kwa kukosa ushahidi wa kutosha.” alisema Mutisya.

Ameeleza kuwa tangu kuasisiwa kwa kitengo hicho cha kusimamia maslahi ya watoto mwaka 2019, kesi 53 za ulanguzi wa watoto zimeamuliwa kortini na watuhumiwa kuhukumiwa huku kesi 23 za unyanyasaji wa kingono kwa watoto zikiamuliwa.

“Kesi za ulanguzi wa watoto tumekuwa nazo na tangu mwezi Julai mwaka 2023 kesi 53 hukumu imetolewa vile vile tumekuwa na kesi 21 za unyanyasaji wa kingono mitandaoni na takwimu hizi ni tangu kuasisiwa kwa kitengo hiki mwaka 2019, hizi ni zile kesi ambazo tumezifuatilia mpaka hukumu ikatolewa. Lakini kunazo kesi nyingi ambazo bado ziko kortini.” alisema Mutisya.

Hayo yanajiri siku chache baada ya utafiti wa shirika la IJM wa mwaka 2021 kuonesha kuwa watoto takriban 7,000 wanahusishwa na biashara za ngono katika kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale.

Erickson Kadzeha