HabariNews

Ilani ya Kukamatwa kwa Mshukiwa wa Ulawiti Mjini Malindi Yatolewa kwa Mataifa zaidi ya 150

Msako mkali unaendelezwa na idara ya usalama kumsaka raia wa Afrika kusini Michael Balentine, mshukiwa mkuu wa ulawiti wa watoto wawili mjini Malindi.

Hii ni baada ya kubainika kuwa mshukiwa huyo alitoroka nchini.

Mueni Mutisya mkuu wa kitengo cha kusimamia maslahi ya watoto katika idara ya upelelezi DCI, tayari serikali imetoa ilani ya kukamatwa kwa Balentine katika mataifa 176 maarufu “Red Notice” kupitia kitengo cha usalama cha kimataifa cha InterPol.

“Tayari tuliwasiliana na kutaka ushirkiano na Interpol imetoa ilani ya ‘Red Notice’ hii ni ya mtu aliyetenda uhalifu na ukatili mbaya na kutorokea nchi nyingine, hii inahusishwa kwa nchi 176 wanachama wa Interpol. Tunajua ni raia wa Afrika Kusini lakini akienda katika nchi mojawapo zilizo na Interpol atanaswa na kupatikana.” Alisema.

Aidha amewataka wananchi kuwa watulivu uchunguzi unapoendelezwa, idara ya upelelezi ikiahidi kuendeleza msako ulimwenguni kuhakikisha mshukiwa huyo anatiwa nguvuni.

Kwa sasa washukiwa wawili wanawake wanazuiliwa kwa madai ya kumsaidia mshukiwa mkuu kuwalawiti watoto hao, mmoja wao akiwa msichana wa umri wa miaka 17 huku kesi ya watoto hao ikiwa mbele ya mahakama ya Malindi.

By Erickson Kadzeha