Uncategorized

LSK Yashinikiza Haki kwa Mwanablogu Aliyetekwa nyara na Kulawitiwa mjini Mombasa  

Chama cha Mawakili nchini, LSK kimekashifu kitendo cha kutekwa nyara na kulawiitiwa kwa mwanablogu mmoja kaunti ya Mombasa.

Kupitia mtandao wake wa X, Rais wa LSK, Faith Odhiambo ametaja kitendo hicho kinaashiria kufeli kwa uongozi nchini na kwamba ni mgogoro mkubwa wa utawala nchini usiozingatia haki za kibinadam, utu na malengo.

Odhiambo ametaja kuwa uhalifu na mwendelezo wa hujuma unaofanywa na watu walio na nafasi uongozini haupaswi kufumbiwa macho akisisitiza kuwa wahusika wa masuala ya uhalifu wanapaswa kukabiliwa kisheria.

LSK sasa inashinikiza Idara ya Upelelezi wa Kesi za jinai (DCI) kuwasaka na kuwafungulia mashtaka wahusika waliotekeleza kitendo cha kikatili kwa mwanablogu huyo kwa haraka iwezekanavyo.

Aidha imeshinikiza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kuwashtaka wahusika wote.

Mwanablogu huyo, Bruce John mwenye umri wa miaka 24 aliyeikashifu kaunti ya Mombasa na hata kumtusi mamake gavana Nassir, anadaiwa kutekwa nyara nyumbani kwake Bamburi mnamo Septemba 12 na kundi la takribani maafisa 20 wa kaunti.

Kundi hilo liliripotiwa kumshambulia na kisha kumlawiti kabla ya kumtupa katika jaa la Mwakirunge alikookotwa na wasamaria wema.

Tayari washukiwa wanne kuhusiana na kesi hiyo wamekamatwa na kufikishwa mahakamani Shanzu walikokana mashtaka yanayowakabili. Wanaendelea kuzuiliwa kwa siku 14 wakisubiri uchunguzi na hatma ya dhamana yao.

By Mjomba Rashid