HabariNews

Mahakama Kuu Yaruhusu LSK Kujumuishwa katika Kesi ya Ulawiti wa Mwanablogu Mombasa

Mahakama Kuu ya Mombasa imekubali ombi la chama cha mawakili nchini LSK la kutaka kujumuishwa katika kesi iliyowasilishwa na Waziri wa Ardhi na ujenzi kaunti ya Mombasa Mohammed Hussein ‘Amadoh’ ya kuzuia kukamatwa kwake.

Hussein aliyetajwa kuwa miongoni mwa washukiwa wakuu waliodaiwa kupanga njama za kumteka nyara, kumjeruhi na kumlawiti mwanablogu tata Bruce John Khajira, alikuwa amepata agizo la mahakama kuzuia kukamatwa.

Akizungumza nje ya majengo ya mahakama hiyo Naibu Rais wa LSK, Mwaura Kabata amesema lengo la kujumuishwa katika kesi hiyo ni kuhakikisha kuwa mwanablogu huyo anapata haki.

Tumekuja leo Kortini kwa kesi ya CEC ambaye alikuwa amepata maelekezo kortini kuzuia kukamatwa kwake, leo mahakama imekubali LSK na Mombasa Law Society kujiunga katika kesi hii, na wajibu wetu kama mawakili ni kuhakikisha kuwa haki inatendeka na Mahakama inatimiza wajibu wake katika haki yake,” akasema Kabata.

Kabata amebaini kuwa Waziri Hussein ‘Amadoh’ amepewa wiki moja ya kutokamatwa japo mahakama inaweza kumfungulia mashtaka na atafika katika makao ya upelelezi DCI atakapohitajika.

Mahakama imempa wiki nyingine moja hatakamatwa, lakini imeeleza kuwa anaweza kufunguliwa mashtaka na anaweza kuitwa na idara ya polisi kuhojiwa.” Alisema.

Kabata aidha amesisitiza kuwa LSK itahakikisha kuwa kitendo sawia na hicho hakitajitokeza tena kokote nchini na kwamba itakuwa funzo kwa wengine walio na njaa za kuendeleza vitisho na ukandamizaji.

BY MJOMBA RASHID