Spika wa Bunge la Kaunti ya Mombasa Aharub Ibrahim Khatri amepuuzilia mbali madai ya kuwepo mgawanyiko katika bunge la kaunti hiyo.
Hii ni kufuatia uvumi wa kuwepo kwa mirengo miwili ya wawakilishi wadi katika bunge hilo, wale wanaoegemea upande wake Spika huyo na wengine wa upande wa gavana Abdulswamad Shariff Nassir.
Spika Khatri amekana madai hayo akisema wawakilishi wadi wote katika bunge hilo wanafanya kazi pamoja na kwa ushirikiano ili kufanikisha maendeleo pasipo kuegemea mirengo wala pande yoyote.
“Mara unasikia kwenye Assembly unaambiwa kuna mgawanyiko sijui kuna timu ya spika na sijui timu ya gavana. Sasa mimi nashangaa saa nyingine nikisikia haya maneno mimi najua sote ni wamoja pale na sioni kama kuna mgawanyiko wowote.”
Spika huyo aliwahiwataka wawakilishi wadi kutekeleza majukumu yao ipasavyo ya kuwawakilisha wananchi wa Mombasa, kutekeleza sera na kufuatilia utendakazi wa kaunti pasipo upendeleo.
“Wengine utasikia MCAs wengine wanauliza kama wewe wataka maendeleo kwako ama mazungumzo. Kama wataka maendeleo ati shikilia upande huu, si unaona hii shida sasa kwa sababu kila mmoja anapata maendeleo lakini tufanye kazi yetu ilie ya oversight kuangalia utendakazi wa kaunti na uwakilishi wa wananchi. Tukifanya haya basi maendeleo yatakuja.” Akasema Khatri.
Spika huyo aidha amekemea suala la unafiki wa viongozi na kuingizwa siasa katika maendeleo, akisema msaada wake binafsi anaojitolea kusaidia wakazi wa Mombasa ni ukarimu na kamwe haihusiani na masuala ya siasa za 2027.
Sisi wenyewe watu wa Mombasa tuna siasa nyingi sana, jambo dogo tunalitia siasa ooh mnamuona yule Spika yuaja vibaya anataka nini. Sasa kama mimi nina uwezo wangu binafsi sijachukua kitu cha Bunge wala kaunti nikisaidia kuna ubaya, nikiona watu wapata shida nisiwasaidie, na wewe mwengine si pia njoo usaidie.
Lakini shida iko kwetu sisi mara nyingi tuna unafiki ati nataka kitu, kitu gani? Kama nataka si nitawaambia, Kila kitu siasa jamani na siasa ya 2027 iko mbali nani anajua atakuwa hai? Tuangalie tuliyo nayo jamani.” Akasema Khatri.
By Mjomba Rashid