AfyaHabariNews

Wasi wasi wa huduma za afya kusambaratika Kilifi.

Wasi wasi wa huduma za afya kusambaratika kwenye hospitali za umma kaunti ya Kilifi unaendelea kusheheni baada ya kamati ya seneti ya uwekezaji wa umma na hazina maalum kufahamu deni la shilingi milioni 303 linalodaiwa bima ya afya ya SHA na hospitali ya rufaa na mafunzo kaunti ya Kilifi.

Serikali ya kaunti ya Kilifi imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuziba mianya ya kuendeleza ufasadi katika hospitali za umma kwa kuanza kutumia mfumo wa kidijitali katika utaoji huduma na kupokea malipo.

Licha ya mafanikio hayo kamati ya seneti ya uwekezaji wa umma na hazina maalum ikiongozwa na mwenyekiti wake Godfrey Osotsi  imeelezea wasi wasi wa huduma za afya kusambaratika kutokana na deni ambalo serikali ya kaunti inadai serikali kuu kupitia bima mpya ya matibabu ya SHA.

Lakini tumeona shida moja ambayo iko kwa mpango wa bima mpya ya matibabu SHA kwamba hospitali hii pekee inadai shilingi milioni 303 kutoka kwa serikali kuu kwa sababu ya deni ambalo halijalipwa. Na hilo ni jambo ambalo linafaa kuzingatiwa linaweza kufanya hospitali nyingi zisiweze kufanya kazi na kusambaratika.” alisema Osotsi.

Kwa mujibu wa gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro deni hilo la zaidi ya shilingi milioni 303 limetatiza utoaji wa huduma kwa wakazi Kilifi kwa kushuhudia uhaba wa dawa kutokana na ukosefu wa pesa za kununua dawa hizo.

Ameongeza kuwa kuchelewa kulipwa kwa deni la bima mpya ya matibabu kumechangia serikali ya kaunti kununua asilimia 42 ya dawa zinazohitajika.

Tukitumia ile bajeti ya serikali ya kaunti mara nyingi tukienda KEMSA tunapata kati ya asilimia 40-42 ya dawa haifiki hata asilimia 45 na hizo asilimia nyingine 55 tunafaa kutafuta mahali pengine. Na tunaweza kutafuta mahali pengine kupitia pesa hizi za SHA na ile michango mingine ambayo serikali ya kitaifa inafaa kupeana kupitia SHA.” alisema Mung’aro.

Kamati hiyo ya seneti ya uwekezaji wa umma na hazina maalum imekuwa ukanda wa pwani kuzuru miradi mbali mbali mjini Mombasa, Kilifi na Malindi.

Erickson Kadzeha.