Imebainika kuwa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) ilikataa kuandikisha walimu zaidi ya 360,000 kutokana na ukosefu wa miundombinu nchi nzima.
Kulingana na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) Nancy Macharia, juhudi zao za kuwaingiza walimu katika SHA zilifeli baada ya kufahamishwa kuwa bima hiyo haina miundo ya kutosha kote nchini kuwahudumia walimu.
Akiongea mbele ya Kamati ya Elimu ya Bunge la Kitaifa, mnamo Alhamisi Bi. Macharia aliwaeleza wabunge kwamba Tume hiyo imekuwa ikitamani kusajili walimu katika mpango wa bima ya umma, lakini hilo halijawezekana kufikia sasa.
“Mwaka jana, tulipokuwa na matatizo na Minet, tulitaka kuwahamisha walimu wetu hadi SHA. Tumetamani kila mara kuwa na walimu wetu chini ya bima ya kitaifa, hata wakati wa siku za NHIF,” akasema.
Kikao hicho kilijiri kujibu malalamishi mengi ya walimu kote nchini, ambao wanaendelea kuteseka kutokana na ukosefu wa matibabu, licha ya kandarasi ya shilingi bilioni 20 ambayo TSC ilitia saini na Minet kutoa bima ya matibabu kwa walimu.
“Tulifanya mkutano na SHA kabla ya kurejesha mkataba wetu na Minet kwa mwaka huu wa mwisho, na walituambia hawana miundo ya kutosha. Walisema watahitaji Ksh.37 bilioni kuandikisha walimu wetu, lakini hata hivyo, hawakuwa tayari kuwachukua mwaka huu,” akaiambia kamati.
Katika kikao hicho cha kamati ya Bunge, Mwenyekiti wake Julius Melly amesimulia kisa cha kutatanisha cha mwalimu ambaye aliwekwa katika kizuizi cha upweke kwa miezi mitatu kwa kushindwa kulipa bili ya hospitali – licha ya kuwekewa bima.
Bi. Macharia, hata hivyo, ametaja ufadhili finyu kuwa kikwazo kikubwa katika utoaji wa bima ya matibabu ya kina, na kuitaka kamati hiyo kutenga rasilimali zaidi.
By Mjomba Rashid