HabariMombasaNewsSiasa

Kunti ya Kilifi yaokoa shilingi Bilioni 1.9 kwa kusuluhisha kesi nje ya mahakama.

Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro ameishauri ofisi ya wakili wa kaunti hiyo kutumia njia ya kusuluhisha kesi dhidi ya serikali ya kaunti hiyo nje ya mahakama, ili kuokoa muda wa kutekeleza mipango ya serikali.

Akizungumza na wanahabari katika makazi yake mjini Kilifi,  Mung’aro amefichua kuwa ofisi yake ilirithi kesi 400 dhidi ya kaunti hiyo, na kupitia mbinu ya kusuluhisha kesi nje ya mahakama gavana huyo anasema kaunti ya Kilifi imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 1.9.

“Kuna kesi moja ambapo hii kaunti ilikuwa inadaiwa shilingi milioni 926 na nikafanya mazungumzo mpaka tukaelewana kulipa shilingi milioni 114, na nyingine ilikuwa ni kesi ya shilingi bilioni 1.1 na ikabidi kesi hiyo tukaipeleka kortini na tukashinda hiyo kesi na kwa sasa kaunti ya Kilifi imeokoa shilingi bilioni 1.9.

“Na sikuwa eti kesi zote zilikuwa za maana, unawezaje kwenda kuwa hoja ya kaunti ambayo kesi hiyo inaweza kuilazimu kaunti kulipa fidia ya shilingi milioni 350 halafu ada ya wakili inakuwa shilingi milioni 900. Je, Inakuingia akilini hiyo? Kwa hivyo nikamwambia wakili ikiwa hujakubaliana nasi basi tukatatue kesi yetu mahakamani.” alisema Mung’aro.

Hayo yamejiri wakati kamati ya seneti kuhusu sheria, inayoongozwa na mwenyekiti wake Mwenda Gataya aliyepia Seneta wa Tharaka- Nithi kueleza kufurahishwa na hatua zilizopigwa na serikali ya Kilifi katika mpangilio wa kuunda sheria zake.

Gataya, ameeleza kuwa kaunti nyingi zinakumbwa na changamoto ya wafanyakazi wasio na tajriba hitajika hali inayosababisha kaunti hizo kusalia nyuma katika kuunda sheria zake huku akizisihi kaunti hizo kuiga mfano wa kaunti ya Kilifi.

“Tutahitaji kuwatuma watu kuja hapa kujifunza. Kwasababu kaunti nyingi zinakumbwa na changamoto ya kuwa na wafanyakazi wasio na tajriba na hawajahitimu na kama kamati ya seneti tuko tayari kusaidia kuzifunza kaunti hizo. Tuko tayari kusaidiana na kaunti yoyote itakayohitaji usaidizi wetu ili tuwawezeshe.” alisema Gataya.

Erickson Kadzeha.