Rais William Ruto ameipongeza Mahakama ya Upeo kwa kile alichokitaja kuwa imara katika kuziongoza mahakama za chini na kuwa msimamizi mkweli wa Katiba ya Kenya.
Akizungumza katika hafla kuadhimisha miaka 12 ya utendajikazi wa Mahakama ya Upeo tangu kuasisiwa kwake, Rais amesema mahakama hiyo imekuwa imara katika mielekeo yake na kusuluhisha masuala tata ya kikatiba, na kuwafanya Wakenya kuwa na imani ya uhakika kwamba haki zao ziko imara thabiti chini ya mchakato wake.
Licha ya kashfa na pingamizi kuelekezewa mahakama hiyo ya juu zaidi nchini hasa kufuatia uamuzi wake wa kubatilisha uamuzi wa mahakama ya Rufaa kuhusu sheria ya fedha ya mwaka 2023, Ruto amesema kinachotia moyo ni ongezeko la imani ambapo idara kuu za Serikali zinashirikiana kuondoa vizingiti vilivyokuwepo awali vya kuoneshana ubabe.
“Kwa hivyo, ni sawa kusema kwamba Mahakama imesimama kama mlinzi mwaminifu wa Katiba yetu, mtetezi wa haki za kimsingi, na nguzo ya demokrasia,” Ruto alisema.
Ameahidi uwajibikaji na kuzitaka kila idara za serikali kuunga mkono Mahakama ya Upeo kuongoza idara Mahakama kufanikisha haki.
Kulingana na Rais Ruto jukumu la mahakama ya Upeo la kutatua mizozo nchini linasalia kuwa ajenda kuu.
Kwa upande wake Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amesisitiza ya kuwepo haja ya uhuru wa Idara zote 3 za Serikali kuheshimiwa sawia na kushirikiana vilivyo kwa idara hizo.
By Mjomba Rashid