Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji amedokeza kuwa Kenya haina vifaa bora vya kulinda mipaka yake.
Akiwa mbele ya kamati ya bunge kuhusu idara ya Ulinzi, Ujasusi na Uhusiano wa Kigeni, Haji amebainisha kuwa vikosi vya usalama vimekosa fedha kwa muda mrefu na haviwezi kupata zana za kisasa za ulinzi.
Amesema kuwa Kenya haiwezi kujilinda kutokana na tishio lililoenea kutoka kwa mataifa jirani, ambalo linaathiri jamii zilizo karibu na mipaka ya Kenya.
Amepigia mfano wa makabila kutoka nchini Uganda ya Karamajong yanayovamia nchini na kutekeleza wizi wa ng’ombe na hata kuvamia ardhi nchini, sawia na kundi la Wanamgambo wa Ukombozi la Oromo kutoka nchini Ethiopia, wanaokalia maeneo ya Kenya kwa mabavu japo changamoto ya kukabiliana nao ni ukosefu wa vifaa.
Aidha Haji amedai kwamba jeshi, kwa mfano, halijapokea vifaa vyao vinavyohitajika kwa miaka 10 iliyopita akiieleza kamati hiyo kuwa makadirio ya bajeti ya sekta hiyo yanahitaji kupewa kipaumbele ili kumaliza mgogoro huo.
Awali NIS ilikuwa imesaka shilingi bilioni 65, lakini bajeti ilipunguzwa hadi shilingi bilioni 51.
Hapo awali, Katibu wa Wizara ya Ulinzi Patrick Mariru alikuwa ameiambia kamati hiyo kwamba ufadhili mdogo pia umeinyima wizara fursa ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Amefafanua kuwa KDF inahitaji takriban shilingi bilioni 2 ili kuajiri mwaka huu, na kuongeza kuwa afisa aliyeajiriwa anahitaji takriban shilingi milioni 2 kwa mafunzo ya miezi 9.
By Mjomba Rashid