MichezoSports

Kilifi United yalambishwa mchanga nyumbani

Kararacha FC wamemkosea mwenyeji wao Kilifi Utd heshima kwa kumpiga ngwala na kumlambisha mchanga kwa mabao mawili kwa moja ugani Water mjini Kilifi kwenye mchuano wa ligi ya kaunti ya Kilifi.

Kwenye mechi iliyochezwa mapema leo, Kararacha FC wamepata bao la ufunguzi mnamo dakika ya 13 baada ya mtanange huo kuanza kupitia Robert Mweri ambae anaendelea kuonesha makali yake akiwa mbele ya lango kwa kupachika bao lake la sita kwenye mechi nne alizocheza.

Aidha Kiba Nasib ameongeza bao la pili katika dakika ya 89 ya ngarambe hiyo na kudidimiza kabisa matumaini ya Kilifi Utd kupata alama baada ya kuandikisha msururu wa matokeo mabaya kwenye ligi hiyo.

Richard Charo Bambanya kocha wa Kararacha FC ameeleza kufurahishwa kwake na ushindi huo huku akiwapongeza vijana wake kwa kujitolea na kupata alama hizo tatu muhimu.

Kusema ukweli nimepoteza nafasi nyingi kwasababu kipindi cha kwanza nimepoteza kama nafasi tano za kufung. Na ningekuwa naye yule winga wangu zile bao zingekuwa zimeingia. Lakini nashukuru kuchukua alama tatu ugenini kwasababu hilo si jambo rahisi. Nawapongeza vijana wangu kwa kujitolea kwao, sasa hivi tunaangazia macho yetu kwa mechi ijayo ambayo tuko nyumbani dhidi ya Hotspurs.” alisema Bambanya.

Licha ya purukushani ya winga matata Ishmael Mohammed Lugo wa Kilifi Utd kuzalisha bao la kukomboa mnamo dakika ya 54 ya mchezo, purukushani hizo hazikutosha kuisaidia meli ya Kilifi utd iliyokuwa inazama.

Samson Jumbe kocha wa Kilifi Utd amesema licha ya vijana wake kujitahidi kwenye mtanange huo changamoto ya majeraha imepelekea timu yake kupoteza mechi ya leo huku akisistiza kuwa kujiamini kupita kiasi kwa vijana wake kumewaponza.

Tumepoteza mechi ya leo licha ya kujitahidi, ila kwa kweli hii mechi imekuwa ngumu kwetu. Imetulemea. Mimi sana nalilia majeraha kwa wachezaji wangu nusu ya kikosi changu ni majeruhi. Inabidi nawalazimisha kucheza kwenye nafasi ambazo sizao ili waokoe jahazi. Jambo jengine ni kwamba vijana wangu wamejiamini kupita kiasi na ndio sababu tumefungwa bao dakika za mwisho. Zile pasi fupi fupi pale langoni zimetuponza.” alisema Jumbe.

Kilifi United wanaoshikilia nambari ya 8 kwenye jedwali wakiwa na alama 4 wanatarajiwa kupambana na Majaoni Sports katika mchuano wao ujao huku Kararacha FC waliokatika nambari ya 5 na alama 10 wakitarajiwa kuwaalika Hotspurs.

Erickson Kadzeha