HabariNews

Rais Ruto awatunuku Kazi za Serikali Aliyekuwa Mwenyekiti wa IEBC Isaack Hassan na Mbunge wa Zamani Jagua

Aliyekuwa Mwenyekiti wa IEBC Isaack Hassan na Mbunge wa Zamani Charles ‘Jaguar’ Watunukiwa Kazi Serikalini; Rais William Ruto akifanya teuzi kadhaa kuimarisha utendakazi Serikalini.

Rais amefanya teuzi mbalimbali katika hatua na azma ya kuimarisha utendakazi wa serikali yake ya Kenya Kwanza.

Amemteua aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi IEBC, Ahmed Isaack Hassan kuwa Mwenyekiti mpya wa Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi, IPOA.

Tangazo hili likitolewa kupitia taarifa kutoka kwa Mkuu wa Utumishi wa umma Felix Koskei, taarifa ambayo imethibitisha kuwa Rais Ruto amewasilisha jina la Isaack Hassan Bungeni ili kuidhinishwa.

Hassan alikuwa mmoja wa wagombea wanane walioteuliwa kuwania nafasi hiyo mnamo mwezi Oktoba, kufuatia mwito wa wazi wa Jopo la Uteuzi wa Mwenyekiti wa IPOA mnamo Septemba 13.

Wanachama katika Bodi hiyo ni pamoja na Anne Wanjiku Mwangi, Dkt. Micah Onyego, Ken William Nyakumita, Boniface Kipkemoi, John Muchiri na Jackline Mwenesi.

Rais Ruto pia amemteua Mwakilishi wa zamani wa Kike kaunti ya Isiolo Rehema Jaldesa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Usawa na Jinsia huku Michael Mbithuka Nzomo akiteuliwa kujiunga na bodi ya tume hiyo kama mjumbe.

Wakati uo huo Rais amefanya mabadiliko katika Tume ya Haki ya Utawala (CAJ) ili kuboresha upatikanaji wa haki, kwa kumteua Charles Orinda Dulo kuwa Mwenyekiti wa CAJ akishirikiana na aliyekuwa mbunge wa Starehe Charles Njagua Kanyi na Dorothy Jemator Kimengech walioteuliwa kujiunga kuwa wanachama wa tume hiyo.

Vilevile Rais Ruto amemteua Gerald Nyoma Arita kwa nafasi ya Naibu Gavana katika Benki Kuu ya Kenya, CBK.

By Mjomba Rashid