Takribani wakazi 198 wa eneo la Kwachocha Malindi kaunti ya Kilifi sasa wanaitaka Serikali kuwafidia mara moja baada ya ardhi yao kuchukuliwa na Mamlaka ya viwanja vya ndege nchini, KAA.
Wakazi hao wanalalamikia hatua ya kutwaliwa kwa ardhi zao na KAA ili kupanua uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Malindi.
Wakazi hao wamewasilisha kesi katika mahakama ya Mazingira na ardhi ya Malindi wakishinikiza kusitishwa kwa mpango wowote utakaoipa Kampuni ya Adani fursa ya kuchukua raslimali za KAA hadi pale watakapofidiwa.
Kupitia wakili wao Vincent Mogaka wakazi hawa wanahofia kuwa huenda wakakosa kupata fidia iwapo Adani itachukua uongozi hasa wa Uwanja wa JKIA muda wowote mwezi ujao na baadhi ya viwanja vya ndege nchini.
Itakumbukuwa katika ombi la kesi iliyowasilisha Oktoba 8 mwaka huu, wakazi hao 198 walisema kuwa mchakato wa ulipaji fidia umejikokota kwa zaidi ya miaka 15 hivyo wanahofia huenda wakakosa fidia kampuni ya Adani itakapochukua uongozi.
Hata hivyo jaji wa Mahakama hiyo Mwangi Njoroge amesema atatoa uamuzi wa kesi hiyo Disemba 3 mwaka huu.
By Mjomba Rashid