Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman ametangaza kujiuzulu.
Whitman ambaye amekuwa katika wadhifa huo tangu mwaka wa 2022 ameelezea uamuzi wake huo katika taarifa mnamo Jumatano, akisema alikuwa amekabidhi barua ya kujiuzulu kwa rais wa Marekani anayeondoka Joe Biden.
Uamuzi wake huo wa kujiuzulu unajiri siku chache baada ya ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi Mkuu wa Urais wa Marekani uliofanyika wiki jana Novemba 4.
“Leo, nimetangaza kwa timu katika Ubalozi wa Marekani kwamba nimewasilisha barua yangu ya kujiuzulu kwa Rais Biden. Imekuwa ni heshima fursa ya kipekee kuwahudumia Wamarekani kupitia kuimarisha ushirikiano na Kenya.” Alisema.
Whitman ameeleza shukrani zake kwa nafasi aliyopewa kuhudumu kama Balozi akiangazia umuhimu wa hatua zilizopigwa wakati wa hatamu zake za uongozi hasa kwa kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa Marekani na Kenya katika sekta na masuala ya afya.
“Ninajivunia kuongoza ajenda inayozingatia watu ambayo itaokoa maisha, kuongeza usalama, na kuunda fursa za kiuchumi kwa Wakenya na Wamarekani. Kuanzia kutoa ufadhili wa dharura ili kupunguza janga la mafuriko mnamo 2023 hadi vita vinavyoendelea dhidi ya malaria, HIV na MPOX, Serikali ya Marekani inatanguliza afya na ustawi wa marafiki zetu nchini Kenya.”
Aidha Balozi huyo amebainisha ushirikiano wa karibu baina ya mataifa haya mawili katika kukuza maendeleo ya kiuchumi, akisema kutokana na juhudi zake za kuimarisha uhusiano uwekezaji wa Marekani hapa nchini Kenya u katika kiwango cha juu kwa sasa.
“Nilipowasili mnamo mwaka 2022, nililenga kupanua uhusiano huu na kauli mbiu yangu ya “Kwa nini Afrika, kwa nini Kenya?” uwasilishaji kwa kampuni za Kimarekani na wajasiriamali. Biashara, ajira, na uwekezaji wa Marekani nchini Kenya uko katika kiwango cha juu kwa sababu ya juhudi zetu,” alisema.
Fauka ya hayo Whitman ametambua zaidi juhudi zinazoendelea za wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani na kuonyesha imani katika mustakbali wa uhusiano kati ya Nairobi na Washington.
By Mjomba Rashid