Mchakato wa kuhakikisha kuwa jamii inaishi kwa amani na kukomesha visa vya mauaji ya wanawake umeanzishwa eneo la Kibarani viungani mwa mji wa Kilifi ili kuleta uwiano na utangamano miongoni mwa jamii.
Taifa likiendelea kushuhudia ongezeko la visa vya mauaji ya wanawake mikakati inaendelezwa eneo la Kibarani kaunti ya Kilifi ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa Fatuma Ramadhani ofisa wa shirika la DADA YANGU wadi ya Kibarani wameanzisha mchakato wa kutoa hamasa kwa vijana wadogo kuhusu kuheshimu, na kuona umuhimu wa kila mmoja kwenya jamii ili kuondoa unyanyasaji na hisia za wengine kubaguliwa.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuleta jamii pamoja na vijana kutoshawishika rahisi kushiriki kwenye visa vya kutoa uhai wa mtu mwengine.
“Humu nchini sasa hivi wanawake tunalalamika sana kutokana na kushuhudiwa kwa visa vingi vya mauaji ya wanawake na ndio sababu tumewaleta pamoja vijana wadogo zaidi ya 100 kuwahamasisha ni jinsi gani tunaweza kuifanya jamii yetu kuwa bora.
“Na tumeanzisha mchakato huu kwa hawa vijana wakiwa bado ni wadogo ndio tuwaeleze kuwa maisha yanafaa kwenda namna hii tunafaa kuwa na mshikamano na kuwawezesha vijana wa jinsia zote ili tusiwe na jamii ambayo ni kama ambae tuko katika mashindano.” alisema Fatuma.
Aidha amesistiza kuwa jamii ikielewa na kujifunza kuheshimu maamuzi ya mtu mwengine, swala la wakazi kutoana uhai kudhalilishana hususan katika mahusiano litaweza kukabiliwa ipasavyo.
Ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana ili kufanikisha mchakato huo.
“Nahisi kwasababu wanaume wetu katika jamii wamekuwa na hulka ya kutaka kuwatawala wanawake na unakuta kuwa mara nyingi wengi wao hawapendi kuambiwa hapana ndio sababu utaona wengine wakiwapiga wake zao vibaya kwa kisingizio kuwa wanawarekebisha. Na maswala kama haya ndio yanayoleta shida zote hizi mpaka wakati mwengine unaskia mtu amemtoa uhai mwengine.” alisema Fatuma.
Erickson Kadzeha