Rais William Ruto ameendelea kutetea baadhi ya maamuzi yake tatanishi aliyoyafnya hadi kufikia sasa, akisema yataisaidia nchi ya Kenya.
Akizungumza mnamo Jumanne katika hafla ya utiaji saini kwa mikataba ya utendakazi wa mawaziri katika ikulu ya Nairobi rais Ruto alitetea maamuzi yake hayo akisema yatazaa matunda hivi karibuni.
Kiongozi huyo wa taifa alisema bima mpya ya afya ya jamii, SHA na mpango wa nyumba za bei nafuu itabadilisha maisha ya Wakenya hivi karibuni.
Alisisitiza liwe liwalo serikali yake itafanikiwa katika kutekeleza na kufanikisha mpango wa bima ya afya ya jamii SHA.
“…Tumeamua safari hii tutalifanikisha na ni lazima iwe sahihi na tutawashangaza wapayukaji…tutafanikiwa na maadui wa Kenya watashikwa na aibu.” Alisema Rais huku akishangiliwa.
Kwa mujibu wa rais Ruto serikali mbili zilizotangulia zilishindwa kubadili sekta ya afya na kutekeleza mfumo jumuishi wa afya kwa wote.
“Tulichukua jukumu la afya kwa wote, na najua marais wawili waliotangulia walijaribu na hawakufaulu vile. Sisi tumeamua tunachukua changamoto hii kwa sababu kuna Wakenya wingi wanakufa na magonjwa ambayo tunaweza kutibu, kuna wengine wanaishia kuwa maskini kwa sababu ya madeni ya hospitali.” Alisema.