Huku ubabe wa ushindani kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti ukiendelea, Bunge la Seneti sasa linatafakari kuanza mchakato sambamba wa kubadilisha Katiba ili kulifanya Bunge hilo kuwa lenye nguvu.
Katika mchakato ambao unaonekana kupata uungwaji mkono wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, Maseneta wanataka sheria zote zilizopitishwa na Bunge la Kitaifa zipitie Bunge la Seneti kabla kuidhinishwa.
Akizungumza katika Bunge la Seneti baada ya kukutana na Maseneta katika kikao maalum, Raila amesema lazima Seneti iruhusiwe kutekeleza jukumu lake katika mchakato wa kutunga sheria sawa na kile kinachofanyika katika bunge la seneti la Marekani.
Odinga amekariri haja ya Seneti kuwa nguvu zaidi kama ilivyo kwa bunge la seneti la Marekani ikizingatiwa kuwa mfumo wao wa katiba na muundo unawiana na uliko nchini Kenya katika misingi ya bunge la seneti.
“Seneti inapaswa kutekeleza jukumu lake, kama vile Bunge la Kitaifa lina jukumu la kutekeleza. Tuna nchi zilizo na muundo sawa wa kikatiba na inafanya kazi vizuri sana. Kwa hivyo tuone Seneti yetu ikifanya kazi kama ile ya USA inavyofanya kazi na tuipe mamlaka na majukumu yanayofaa,” akasema Raila.
Akionekana kupinga mpango wa Bunge la Kitaifa kubadilisha Katiba na kuidhinisha Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneobunge (NG-CDF) katika Katiba, Raila amesisitiza kuwa Bunge lazima tu kutekeleza majukumu yake kulingana na Katiba.
Hata hivyo Odinga amesisitiza haja ya mabunge hayo kushirkiana akisema kuwa Bunge la Kitaifa halipaswi kuwa na hofu yoyote na Seneti katika utekelezaji wa majuku yao bali tu uwajibikaji.
“Bunge la Kitaifa na Seneti huunda Bunge na jukumu lao ni kuwakilisha, kutunga sheria na kusimamia na majukumu hayo ni muhimu sana. Watendaji hutumia sheria zilizopitishwa na Bunge kutawala nchi na Idara ya Mahakama inaitafsiri, hivyo ndivyo tunavyotaka iwe,” Raila alisema.
Maseneta pia wameapa kutupilia mbali mpango wa marekebisho ya katiba unaoongozwa na Wabunge wa Bunge la Kitaifa, ambao unalenga, miongoni mwa mambo mengine, kusisitiza Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) katika Katiba.
Wakizungumza baada ya mkutano huo wa saa mbili na Raila, Maseneta hao wameelezea hofu ya kuwepo kwa nguvu ambazo zinalenga kurudisha nyuma mafanikio ambayo yamepatikana katika ugatuzi.
Kulingana na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, Seneti imeamua kukataa Hazina ya Seneti ya Uangalizi ambayo imependekezwa kwenye Mswada wa Marekebisho ya Bunge la Kitaifa, ikidai kuwa hazina hiyo inatumiwa kama chambo cha kupitisha hazina haramu ya NG-CDF.
By Mjomba Rashid