Bunge la Kitaifa limeitaka mahakama kuruhusu shughuli ya kuwakagua watu saba walioteuliwa na Rais William Ruto katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuendelea bila kukatizwa.
Kulingana na Bunge hilo hatua ya Mahakama kuingilia kati kuzuia ukaguzi na uidhinishwaji wa saba hao ni mapema mno na kinyume cha maslahi ya umma.
Katika kujibu kesi iliyowasilishwa kupinga uteuzi wa wateule saba hao, Bunge la Kitaifa linasema kuwa kusimamisha mchakato huo kunadhoofisha ushiriki wa umma na kuvuruga zoezi la katiba lililowekwa kwa wakati.
Kupitia Naibu Karani Jeremiah Ndombi, Bunge linashikilia kuwa maagizo ya muda yaliyotolewa na Jaji Lawrence Mugambi mapema wiki hii hayakuwa na uhalali, kwani walalamishi walikosa kuwasilisha kesi kali ya kutaka kuachiliwa huru.
Ikumbukwe kuwa Jaji Mugambi alisimamisha mchakato wa kuwaidhinisha saba hao hadi Mei 29, 2025, atakapotoa uamuzi.
Hata hivyo, Bunge linasema kwamba Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) lazima iwasilishe ripoti yake kufikia Mei 27, kwa mujibu wa ratiba ya siku 28 iliyowekwa katika Sheria ya (Idhini ya Bunge) kuhusu Uteuzi wa Umma.
Aidha kulingana na Bunge, walalamishi hao; Kelvin Roy Omondi na Boniface Mwangi, hawajaonyesha kwamba watapata madhara yasiyoweza kurekebishwa iwapo uhakiki utaendelea.
Bunge pia linasema kuwa masuala yaliyoibuliwa katika ombi hilo, ikiwa ni pamoja na madai ya uteuzi kinyume cha katiba na kutostahiki kwa wateule, yanaweza kushughulikiwa ipasavyo wakati wa mchakato wa uhakiki unaoendelea.
Waliowasilisha kesi hiyo wanadai kuwa Rais alitenda wajibu huo kinyume cha sheria na kwamba wanne kati ya walioteuliwa hawakukidhi vigezo vya stahikifu.
Wagombea walioibua pingamizi ni pamoja na mwenyekiti wa IEBC anayependekezwa Erastus Edung Ethekon, pamoja na Makamishna Hassan Noor Hassan, Mary Karen Sorobit, Anne Nderitu, Moses Mukwana, Francis Odhiambo, na Fahima Araphat Abdallah.
By Mjomba Rashid