HabariNews

Maafisa wa Afya wa Hospitali za Kibinafsi Walalamikia Kukandamizwa na Serikali ya Kaunti ya Mombasa

Wahudumu wa Afya wa hospitali za kibinafsi kaunti ya Mombasa wanalalamikia kukandamizwa na Serikali ya kaunti hiyo kupitia makato ya ushuru na ulipiaji vibali wanaodai si halali.

Wahudumu hao kupitia Muungano wao wa Hospitali za Kibinafsi za Mijini na Mashinani, RUPHA umedai kuhangaishwa na maafisa wa kaunti ya Mombasa wanaowatoza kodi za vibali vya biashara (single business permit) licha ya kuwepo kwa agizo la mahakama la mwaka 2021 lililositisha hilo.

Wahudumu hao wanadai kuhangaishwa na baadhi ya maafisa wa kaunti ambao huwachukulia vifaa vyao na mashini za kazi wanaposhindwa kutekeleza malipo hayo wanayodai ni kinyume cha sheria.

Wakizungumza na waandishi wa habari  mnamo Alhamisi Novemba 28 wahudumu hao wakiongozwa na mwenyekiti wao Dkt. Brian Lishenga walisema serikali ya kaunti ya Mombasa inawatoza ushuru maradufu kinyume cha sheria na sasa wanataka mazungumzo kati yao na serikali ya kaunti kufanyika ili kutatua suintofahamu inayozingira kliniki  na kutafuta suluhu la kudumu badala ya vuta ni kuvute na ubabe usiokuwa faida kwa mwananchi wa kawaida .

 “ Kwa hivyo sisi tunasema kwanza majadiliano. Wakubali tuongee maana kuna amri iliyoko ya mahakama. Na ikiwa hawatataka kuongea, basi tutachukua mbinu za kisheria dhidi yao.” Alisema Dkt. Lishenga

Aidha walibua madai ya unyanyasaji na dhuluma kutoka kwa maafisa wa kaunti wanaowashurutisha kulipia kibali cha kuendesha huduma katika zahanati zao wakisema hali hiyo imefanya huduma za matibabu kuwa ghali mno kwa mwananchi wa kawaida.

 “Hiki Kibali cha kibiashara kina ushuru maradufu. Tayari wanachama wetu wanalipa ushuru mwingi kwa idara husika na zinazofaa kwa mujibu wa sheria na sasa kuleta ushuru mwingine ni hujuma. Hata huduma wanazofaa kupata wananchi hawapati.” Aliongeza Lishenga.

 Muungano kadhalika uliiomba serikali ya kaunti ya Mombasa kufuata na kuheshimu amri ukiwataka maafisa wa serikali ya kaunti ya  Mombasa  maafisa hao kutohujumu sheria na amri iliyotolewa na Mahakama la visivyo wawachukulie hatua kazi za kisheria.

 “Ikiwa kaunti ya mombasa itaendelea kudhulumu wahudumu hawa basi itabidi tuwachukulie hatua maafisa husika wanaotumika kutekeleza hila hiyo. Wewe kama afisa wa kaunti  utaingia katika hospitali ya kibinafsi na hudhulumu ama hubebe mitambo na tujue  kitambulisho chako, au utambuliwe wewe tutakuchukulia hatua kali za kisheria.” Alisema Lishenga

Kauli ya wanachama wa muungano huo inajiri huku madai yakiibuliwa kwamba serikali ya kaunti ya Mombasa inawatoza ushuru maradufu kinyume cha sheria na pia amri ya mahakama ya 2021 inayozizuia kaunti zote kutoza ushuru wanachama wa muungano huo.

BY ISAIAH MUTHENGI