Rais William Ruto amewaonya zaidi ya Maafisa wa mashirika ya Kiserikali waliokiuka agizo la kuhamisha huduma zao kwenda mfumo wa kidijitali kupitia mtandao wa E-Citizen ili kuimarisha uwazi na utendakazi mwafaka.
Akizungumza mnamo Alhamisi Novemba 28 katika maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kuzinduliwa upya kwa jukwaa la e-Citizen, Rais Ruto aliwaamuru Wakuu 34 wa mashirika ya serikali kuhakikisha wanafanikisha utoaji wa huduma zao na malipo yanapatikana katika mfumo mmoja wa jukwaa la kidijitali la e-Citizen ndani ya siku 7 zijazo la sivyo wafutwe kazi.
“Mashirika haya yangali hayajatii na kufuata maagizo yangu kwamba huduma zao, malipo na mapato yao lazima yawe katika jukwaa la e-citizen. Wana wiki moja kutii maagizo hayo; Vinginevyo wanajua wanachopaswa kufanya, wanaweza kuuona mlango (kuacha kazi).” Alisema Rais.
Rais ameyataja Mashirika ambayo amedai yanahujumu na kulemaza juhudi za uwazi na uwajibikaji wa ukusanyaji mapato katika sekta ya umma.
Miongoni mwa mashirika hayo ya kiserikali ni Mamlaka ya Bandari ya Mombasa KPA, Kenya Power, Shirika la Kawi EPRA, Shirika la umeme mashinani REREC, Kenye RE, Bodi ya Mitihani ya Kitaifa KNEC, pamoja na bodi nyinginezo.
Kiongozi huyo wa taifa amesema mashirika hayo yamechelewa kuhamisha huduma ili kuzuia ufujaji wa fedha na kwamba baadhi wamekuwa wakitumia njia fiche mbadala kufanikisha malipo kinyume cha sera ya serikali.
By Mjomba Rashid