Rais William Ruto amewakashifu baadhi ya Wakenya na viongozi aliowataja kuwa wanapinga miradi yake yote katika sekta mbalimbali.
Akizungumza mnamo Jumanne huko Voi kaunti ya Taita Taveta katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa Devki wa kuchakata chuma, rais amewataja watu hao kama ‘Pepo mchafu’ na walio na nia mbaya na maendeleo ya taifa.
Rais amesema wale wanaopinga mipango na miradi mingi ya serikali hawana uzalendo wa taifa, akidai wanaeneza jumbe za kuvunja moyo na kupinga miradi muhimu kama vile ujenzi wa nyumba za bei nafuu, bima ya afya kwa wote Taifa Care maarufu SHA, ufadhili mpya wa masomo ya vyuo vikuu miongoni mwa mingine.
“Nataka niulize Wakenya tafadhalini, kuna pepo chafu ya kupinga kila kitu. Kiwanda kama hii, affordable housing wanaipinga, chanjo ya ng’ombe kuondoa magonjwa, kubadilisha mfumo ndo tuweze kuokoa university zetu wanaipinga, mambo ya afya wanaipinga. Miradi yoyote ya serikali, sasa mimi nauliza hii pepo chafu. Jameni, Imefika wanapinga ata matoleo kanisani, jameni surely, what is this, surely. yani pepo ya kupinga kila kitu,” alisema.
Kiongozi huyo wa taifa aliwataka viongozi wa eneo hilo wanaopinga mradi wa kiwanda cha Devki kujiepusha na fitina na kukaa kando kuruhusu mradi huo wa kiwanda cha chuma ufaidi maelfu ya vijana kiajira.
Kauli ya Rais iliungwa mkono na Waziri wa madini na uchumi wa majini, Hassan Ali Joho aliyekashifu wanaotumia itandao mbalimbali kupinga miradi na ajenda za serikali, akidai kuwa yu tayari kukabiliana nao.
“Hii nchi haiwezi kuendelea kupitia mtandao, haiwezekeni. Kwani hii kazi imezinduliwa hapa ni facebook, ni twitter ama ni tiktok? Si ni watu si ni kazi imefanywa kwa ground, jana kuna watu walikua ati kunisalaimia na shilingi moja moja, nawambia kujeni tumeni 100 ama 200, na mimi nawangojea…” alisema.
By Mjomba Rashid