HabariNews

Kampuni Ya Skyward Yazindua Safari Ya Kwanza Ya Ndege Kutoka Mombasa – Dar-Es Salaam

Kuna haja Serikali kupitia mamlaka husika ya Uchukuzi na usafiri wa anga kuzijengea uwezo kampuni ndogo za ndege ili kuwafungulia masoko zaidi ya kuhimili ushindani wa kibiashara.

Haya ni kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kampuni ya ndege ya Skyward Express Capt. Mohammed Abdi, akizungumza katika Hafla ya uzinduzi wa safari ya kwanza ya kampuni hiyo ya ndege kutoka uwanja wa Kimataifa wa Moi mjini Mombasa hadi Dar es Salaam, Tanzania.

Capt. Abdi amesema kando na kushinikiza kufunguliwa anga huru kwa ndege za kimataifa kuwasili kwa minajili ya kuimarisha utalii, kuna haja kubwa kuzijengea uwezo kampuni za ndege za hapa nchini na kuziunga mkono kwa kuziimarisha vilivyo ili kuleta ushindani wa kibiashara na maendeleo.

Mwenyekiti huyo ametaja uzinduzi wa safari za ndege za kampuni hiyo kutoka Mombasa hadi Dar es Salaam, Tanzania kuwa afueni na mwanga wa matumaini kwa abiria sawia na kuimarika kibiashara na maendeleo ya kaunti ya Mombasa.

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) Caleb Kositany amesifia hatua hiyo akisema itafungua na kukuza sekta ya utalii sawia na kukuza biashara huku akisema wanapania kupanua na kuendeleza maeneo ya viwanja vya ndege ili kukidhi mahitaji ya wasafiri na mashirika mengine ya usafiri wa ndege.

Kwa upande wake Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharrif Nassir akiunga mkono uzinduzi wa safari hizo kisema uwepo wa safari za ndege kuelekea maeneo mbalimbali kunasaidia pakubwa kukuza sekta ya utalii na kufungua eneo la Pwani kibiashara na kimaendeleo.

Uzinduzi wa safari za ndege hiyo umetajwa kuwa afueni ambapo ndege za Skyward Express zitakuwa zikifanya safari zake mara mbili kwa wiki.

Safari hizo za ndege kutoka uwanja wa Moi mjini Mombasa hadi Julius Nyerere, Dar es Salaam nchini Tanzania zitakuwa kila Jumatano na Jumamosi abiria wakilipa kiwango cha chini cha shilingi 16,610.

By Mjomba Rashid