HabariNews

Vijana wahimizwa kuepuka Uhalifu na badala yake kukumbatia Elimu na kozi za Kiufundi

Vijana kutoka kaunti ya Mombasa wamehimizwa kukumbatia elimu kama zana ya kuwakomboa kutokana na janga la uhalifu na utumizi wa dawa za kulevya.

Kwa muda mrefu sasa uhalifu na utumizi wa mihadarati umeendelea kuwa tatizo sugu hasa katika ukanda wa Pwani huku idadi kubwa ya vijana wakitokomea katika janga hilo na kukiweka kizazi kijacho katika hatari ya  kuangamia.

Mwenyekiti wa mradi wa LAPSSET Ali Menza Mbogo aliwashauri vijana kulipa umuhimu suala la elimu kwani elimu ina uwezo mkubwa wa kuyabadilisha maisha ya vijana.

Akizungumza na wanahabari kwenye tamasha la talanta na uigizaji ‘Pwani Talentika’ iliyoandaliwa na Chuo cha Kiufundi cha Pwani eneobunge la Likoni kaunti ya Mombasa, Mbogo alisisistiza haja ya kuwekeza katika elimu akisema kwamba kizazi kilichoelimika hakiwezi kuwa muda wa kujishughulisha na masula ya kupotoka.

 “Uhalifu haulipi. Ndio maana mimi nawaomba vijana wetu tulikumbatie suala la elimu,” alisema.

Ali Menza Mbogo, Chairman LAPSSET Lamu county

Mbogo ambaye pia alikuwa Mbunge wa Kisauni, aidha aliwahimiza vijana kusomea ujuzi na kupata elimu ya kiufundi ili waweze kujiendeleza kimaisha.

Fauka ya hayo aliwarai viijana hata wale wenye stashahada kuzingatia kuongeza ujuzi katika vyuo mbalimbali vya kiufundi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata ajira wanapowasilisha maombi yao ya kazi.

Wakati uo huo Mkurugenzi wa chuo cha kiufundi cha Pwani Technical College kilichoandaa tamasha hilo, Suleiman Mwachuo aliwasihi vijana wenye vipaji kutumia vipaji vyao kujibunia ajira badala ya kijihusisha na masuala ya uhalifu.

Mwachuo aidha aliwasihi vijana eneo la Likoni na kote kaunti ya Mombasa kukumbatia kozi na taaluma za kiufundi kama njia moja wapo ya kujiwekea mazingira bora ya kupata ajira katika sekta mbalimbali.

Itakumbukwa kuwa eneobunge la Likoni limekuwa likishuhudia visa vya uhalifu vinavyotekelezwa na magenge ya vijana.

Katika tamasha hilo vijana wenye wenye vipaji mbalimbali vikiwemo uanamitindo, uimbaji, densi, uigizaji miongoni mwa vingine walipata fursa ya kuonyesha weledi na vipaji vyao sawia na kujiburudisha katika kipindi kilichosheheni shamrashamra za sherehe za mwisho wa mwaka.

Tamasha hilo liliandaliwa na chuo hicho kwa ushirikiano na washikadau na mashirika mbalimbali kaunti ya Mombasa.

Na Mohammed Mwajuba