HabariNewsSiasa

Odinga Akashifu Visa vya Utekaji Nyara; IPOA ikijitokeza kuanzisha Uchunguzi

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa visa vya utekaji nyara vinavyoendelea kushuhudiwa nchini.

Odinga amesema matokeo hayo ambayo yamekithiri mwaka huu yanafaa kuangaziwa kwa haraka na serikali la sivyo yatahatarisha usalama wa taifa.

Odinga aidha amebaini kwamba mbinu za kutumia utekaji nyara kuwauzia wananch woga zimepitwa na wakati huku akitaka wote watakaohusishwa na ukatili kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Kufikia sasa, Bernard Kavuli, Peter Muteti na Billy Mwangi wameripotiwa kutoweka na kanda za video zikionesha wakichukuliwa kwa nguvu zilionekana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Vijana hao walitoweka baada ya kutoa machapisho yenye utata kwenye mitandao ya kijamii.

Utekaji nyara huo umezua taharuki kote nchini Kenya, ambapo polisi wanalaumiwa kwa kuwachukua kwa nguvu watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Mnamo Jumatano Mamlaka Huru ya Kusimamia utendakazi wa Polisi (IPOA) ilisema imepokea ripoti za utekaji nyara unaotekelezwa na polisi.

Kulingana na IPOA, imepokea ripoti za kutekwa nyara kwa watu 5 kutoka Kajiado, Nairobi na Embu.

Mamlaka hiyo iliongeza kuwa iwapo wanachama wowote wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) watapatikana na hatia, hatua zitachukuliwa dhidi yao.

IPOA sasa ikimtaka Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja kuchukua hatua ili kukomesha visa vya utekaji nyara vinavyozidi kuongezeka.

By NEWS DESK