HabariNews

Wapelelezi Wataka Korti Iwazuie kwa siku 21 Zaidi Washukiwa wa Mauaji ya Afisa Mkuu wa IEBC Mombasa

Maafisa wa upelelezi mnamo Jumanne Januari 14, waliwasilisha ombi la kutaka washukiwa wa mauaji ya Afisa Mkuu wa IEBC kaunti ya Kilifi Aisha Abubakar, wazuiliwe kwa siku 21 zaidi.

Maafisa hao walitaka muda huo ili kukamilisha uchunguzi dhidi ya washukiwa hao watatu waliokamatwa hapo siku ya Jumatatu.

Kesi hiyo iliwasilishwa mahakama ya Shanzu huku washukiwa wawili kati ya watatu wakiwasilishwa mbele ya hakimu mkuu mkaazi Leah Juma huku mshukiwa wa tatu Issa Omar aliyekamatwa pamoja nao amekosa kufikishwa mahakaman.

Aidha mahakama imeagiza mshukiwa Brian Shikuku kubadilishwa jina na kutambuliwa kama Joseph Sande baada ya kubainika kuwadanganya maafisa wa polisi wakati wa kukamatwa kwao.

Joseph alifikishwa kortini humo pamoja na Brian Templa Oyare wakisubiri uamuzi wa mahakama kuhusu ombi hilo la kuzuiwa kwa siku 21 zaidi.

Washukiwa hao wanadaiwa kumwua afisa mkuu huyo wa IEBC nyumbani kwake Utange, Kisauni kaunti ya Mombasa yapata juma moja lililopita.

By Mjomba Rashid