Maafisa wa kusimamia mtihani wa kitaifa wa darasa la nane KCPE katika kaunti ya Lamu wametakiwa kuwajibika ili kufanikisha mtihani huo ambao umeanza hii leo.
Mkurugenzi wa idara ya elimu kaunti ya Lamu Joshua Kaaga pamoja na maafisa wengine wa serikali wamesema ufanisi wa mtihani huo unategemnea ushirikiano wa wadau wote hivyo basi kila mmoja atekeleze majukumu yake kikamilifu.
Wameyasema haya wakati walipokuwa wakiwahutubia maafisa wa polisi pamoja na maafisa watakaosimamia mitihani katika shule mbalimbali baada ya kufunguliwa kwa kasha lililokuwa likihifadhiwa mtihani hiyo kisiwani Lamu.
Kwa upande wake kamishina wa kaunti ya Lamu Irungu Macharia amesema mtihani huo umefunguliwa kwa wakati ufao huku akisisitiza kuwa hali ya usalama iko shwari kwa ajili ya mtihani huo.
Aidha ametoa onyo dhidi ya wanafuzni kujihusisha na udanganyifu akisema kuwa serikali haitaruhusu visa vyovyote vya udanganyifu kwenye mtihani huo.