HabariNews

Matokeo ya KCSE kutangazwa rasmi leo, huku shule zikifunguliwa kwa muhula wa tatu….

Matokeo ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE yanatarajiwa kutolewa rasmi leo baada ya waziri wa elimu profesa George Magoha kufunga rasmi zoezi la kusahihisha mtihani huo juma lililopita katika shule ya upili ya kitaifa ya wavulana ya Starehe.

Zoezi hilo lilikumbwa na utata huku migomo ya waalimu waliokuwa wakisahihisha mtihani huo ikishuhudiwa kutokana na waalimu hao kukosa marupurupu.

Watahiniwa wapatao laki nane waliandika mtihani huo ulioahirishwa kutokana na janga la corona kubisha hodi humu nchini.

Haya yanajiri huku shughuli za masomo zikirejelewa mapema leo, kwa muhula wa tatu baada ya likizo ya majuma saba kukamilisha kalenda ya masomo ya mwaka 2020 iliyotatizwa na uwepo wa janga la corona.

Aidha ni muhula tofauti na mihula mingine iliopita kwani muhula huu utakosa uwepo wa wanafunzi wa gredi ya 4, darasa la nane na kidato cha nne ambao kwa sasa wako nyumbani baada ya kukamilisha mitihani yao ya kitaifa.

Wizara ya elimu inatazamiwa kutoa kalenda ya masomo ya mwaka 2021 mwishoni mwa mwezi julai mwaka huu.

By News Desk