Mamlaka ya maendeleo ukanda wa Pwani CDA imewataka wakaazi kutumia mvua inayoshuhudiwa na kupanda mimea ya chakula ili kuepuka janga la njaa katika siku za usoni.
Akizungumza na kituo hiki mjini Malindi mwenyekiti wa mamlaka hiyo Philip Charo amewashauri wakulima kupanda mimea ya muda mfupi ili kufaidi mvua inayoshuhudiwa kwa sasa.
Charo anasema janga la njaa linaloshuhudiwa katika maeneo ya Ganze, Rabai na Magarini linaweza epukwa endapo wakulima watatumia kilimo hiki vyema.
Wakati uohuo mwenyekiti huyo amefichua kuwa mamlaka hiyo inalenga kuchimba mabwawa ili kuhifadhi maji ya mvua kwa matumizi ya wakulima katika siku za usoni.
Hata hivyo amewataka wakaazi kutumia mbinu mbali mbali kuhifadhi maji ili waweze kutumia endapo kutashuhudiwa kiangazi.
Kauli ya mamlaka hiyo inajiri huku eneo la pwani likishuhudia mvua nyingi katika kipindi cha wiki mbili sasa licha ya kushuhudia kiangazi kilichopelekea baa la njaa na kupelekea wakulima kupoteza mimea na mifugo.
BY NEWSDESK