Jaji Mkuu Martha Koome amewahakikishia maafisa wa mahakama kote nchini usalama wao kufuatia shambulizi linaloshukiwa kuwa la al-Shabaab katika kaunti ya Lamu usiku wa hapo jana.
Maafisa kadhaa wa mahakama waliachwa na majera baada ya kupigwa risasi na washukiwa wa Alshabaab walipokuwa wakielekea katika mji wa Garsen kutoka Mahakama ya Rufaa ya Kipini usiku wa jana katika eneo la Lango la Simba, Kaunti ya Lamu.
Jaji Koome amedokeza kuwa ameagiza Kitengo cha Polisi cha Mahakama kuchunguza hali ya usalama ya majaji, maafisa wa mahakama na wafanyakazi ili kuchukua hatua zinazofaa ili kuhakikisha usalama wao.
Amethibitisha kuwa waliojeruhiwa katika shambulio hilo ni Hakimu Mkuu Mwandamizi Paul Rotich, karani wa Mahakama Boy Njue, Frank Sirima kutoka afisi ya (ODPP), Konstebo wa Polisi Moses Bett na Willis Mgendi pamoja na dereva wao Abel Barisa.
Koome ameagiza waathiriwa hao wahamishwe hadi Nairobi kwa uangalizi maalum zaidi.
Ametoa sifa kwa inspekta jenerali wa polisi Hillary Mutyambai kwa hatua ya haraka aliyochukuliwa na idara ya usalama kwa kudhibiti athari Zaidi kutokana na washukiwa hao.