HabariMombasaNews

ASILIMIA 18.7 YA VIJANA WANAOTUMIA DAWA ZA KULEVYA WATAJWA KUWA KATIKA HATARI KUBWA.

Asilimia 18.7 ya vijana wanaotumia dawa za kulevya kwa kujidunga sindano wametajwa kuwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi kaunti ya Kwale.

Haya ni kwa mujibu wa mkurugenzi wa shirika la kijamii la watumizi wa mihadarati kaunti hiyo (KWANPUD) Ahmed Mohammed anayetaka hamasa zaidi kutolewa kwa vijana ili kuzuia maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.

Kulingana na Mohammed, maambukizi miongoni mwa vijana ni ya kutamausha kufuatia utafiti wa baraza la kitaifa la kupambana na Ukimwi (NSDCC) unaonyesha kuwa asilimia 3.2 ya wakaazi wa Kwale wanaishi na ugonjwa huo.

Kwa upande wake mshauri wa maswala ya kiafya kutoka baraza la kitaifa la vijana (NYCC) Rose Otaye amesema kuwa Kenya imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Otaye amesema kuwa tayari mashirika mbali mbali nchini yamepokea msaada wa kifedha ili kupunguza maambukizi hayo miongoni mwa waraibu.

BY EDITORIAL DESK