Uncategorized

MAHAKAMA YATUPILIA MBALI KESI YA KUPINGA USHINDI WA DIWANI KAUNTI YA KILIFI.

Mahakama ya mjini Kilifi imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa kwake na Matano Athman Tawfiq kupinga ushindi wa diwani wa Sokoni, Ray Katana Mwaro kwenye uchaguzi mkuu uliopita kwa kukosa ushahidi wa kutosha.

Mwanahabari wetu Erickson Kadzeha kutoka kaunti ya Kilifi na maelezo ya kina.

Akizungumza muda mchache baada ya uamuzi wa kesi hiyo kutolewa na hakimu mkaazi wa mahakama ya Kilifi Geofrey Kimang’a, Mwaro ameeleza kuwa uwepo wa kesi hiyo mahakamani umetatiza kwa kiwango kikubwa utendakazi wake.

Amesema kilichosalia sasa ni kuwafanyia kazi wakazi kwa kutekeleza miradi ya maendeleo aliyoahidi wakati wa kampeni zake.

Baadhi ya madiwani waliondamana na Mwaro, wakiongozwa na diwani wa Mnarani Juma Chengo pamoja na wa Kibarani Moses Furaha Keah wameeleza kuwa ni wakati mwafaka wa wakazi kupokea huduma walizoahidiwa.

Aidha wameishukuru mahakama kwa kufanya uamuzi wa haki kwa wakazi wa Sokoni, kwa kushikilia chaguo lao.

Ray Katana Mwaro alipata kura  3099 huku mpinzai wake ambaye ndiye aliwasilisha kesi ya kupinga maotokeo hayo  Matano Athman Twafik akipata kura 3097 wakati wa uchaguzi mkuu ulipotia.

 

BY ERICKSON KADZEHA