Siku ya kuadhimisha uhuru wa vyombo vya habari ikiadhimishwa kote
ulimwenguni kila tarehe 3 Mei, shirika la wanahabari nchini KCA
limewahimiza wadau mbali mbali kushirikiana vyema na wanahabari ili
kurahisisha utendakazi wao.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya leo ikiwa ni kuunda mustakabali wa haki za
uhuru wa kujieleza kama kichocheo cha haki nyingine zote za binadamu.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo mjini Kilifi mwenyekiti wa
shirika la wanahabari nchini KCA ukanda wa pwani Baya Kitsao amekosoa
hatua ya vyombo vya dola kuwazuia na kuwahangaisha wanahabari kuangazia
matukio, hasa yale yenye utata akieleza kuwa ni ukiukaji wa uhuru wa
vyombo vya habari.
Kitsao ameitaka wizara ya usalama wa ndani kuhakikisha inaweka mikakati
ya kuona kwamba uhuru wa vyombo vya habari haukiukwi.
Kitsao hata hivyo amekikashifu kitendo cha wafuasi wa kanisa la New Life
Prayer Center cha kuwafurusha waandishi wa habari wa shirika moja nchini
waliokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Ameongeza kuwa wanahabari wengi wamekuwa wakikumbwa na changamoto za
msongo wa mawazo kutokana na kulipwa mishahara duni, huku akiwarai
wamiliki wa vyombo vya habari kuwalipa mishahara mizuri wafanyakazi wao
ili kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
BY ERICKSON KADZEHA.