HabariNews

Uhaba wa walimu katika Shule za umma Eneobunge la Kilifi Kusini wachangia kudorora kwa elimu

Changamoto ya uhaba wa walimu katika shule nyingi za umma, hususan eneo bunge la Kilifi kusini imetajwa kuchochewa na siasa kwenye wizara ya elimu.

Akiongea wakati wa kutoa takriban shilingi milioni 20 za basari kwa wanafunzi zaidi ya 2000 wa vyuo vya kati na vyuo vikuu, mbunge wa Kilifi kusini Ken Chonga, amesema uhaba wa walimu katika shule za umma eneo hilo umezidisha changamoto katika sekta ya elimu.

 

Chonga anaihimiza Wizara ya elimu kutatua shida hiyo wala sio kuitilia siasa akisema kuwa shule nyingi katika eneobunge la Kilifi zina uhaba wa walimu wanaolazimika kushughulikia wanafunzi wengi kuliko inavyostahiki.

 

“Ukiangalia the teacher student ratio hapa Kilifi South utaona mwalimu mmoja ameachiwa zaidi ya watoto 100 na walimu walioajiriwa na serikali ni 6 au 8. Mimi kwangu nachukulia ni siasa inaendelea katika sekta ya elimu, itakuaje shule zingine ziwe na walimu excess halafu zingine hazina walimu?” Akasema Bw. Chonga.

 

Aidha ameeleza masikitiko yake kuwa hali hiyo imewalazimu wazazi kubandikwa jukumu la kuwalipa walimu wanaoajiriwa na halmashauri za shule kukabiliana na upungufu huo, jambo analodai kuwa limekuwa mzigo kwa wazazi na kuchochea wanafunzi wengi kurejeshwa nyumbani kwa kufeli kulipa ada hizo.

 

 

“Na kama shule hazina walimu inaforce shule ziajiri walimu na wazazi ndio watakaolipia. Hali zi ni hizi tunazozijua, gharama ya maisha iko juu, watu wanalala njaa. Na leo hii mzazi yule anatarajiwa atoe takribani shilingi elfu 5 kugharamikia matumizi ya shule, hapo mzazi anashindwa, ndio unapata watoto kila mwezi wanarudishwa nyumbani.” Akalalamikia Mbunge huyo.

 

Chonga ameitaka serikali kutafuta njia mbadala ya kukikidhi mahitajio ya elimu katika maeneo hayo na kunusuru viwango vya elimu vinavyoonekana kudorora.

BY ERICKSON KADZEHA