Asilimia 27 ya mapato ya kaunti ya Mombasa yanatokana na Bandari huku asilimia 4 pekee yakitokana na utalii.
Haya ni kwa mujibu wa Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir ambaye alibaini kuwa kukosekana kwa mfumo wa anga huru (Open sky policy) ndiko kumechangia pakubwa hali hiyo duni ya mapato.
Kulingana na Gavana Nassir mfumo huo unaoruhusu safari za moja kwa moja za ndege za kimataifa kuja Mombasa kutoka ughaibuni, ulileta natija katika maendeleo na ukuaji wa uchumi wa Mombasa na Pwani kwa jumla kwa kuimarisha idadi ya watalii nchini na biashara.
Aliyasema haya Jumanne Agosti 22, alipotembelewa afisini mwake na Waziri wa masuala ya kigeni kutoka taifa la Denmark Lars Løkke Rasmussen aliyeandamana na balozi wa taifa hilo hapa nchini Ole Thonke.
“Asilimia 27 ya mapato ya kaunti yanatoka kwenye bandari huku asilimia 4 pekee inatokana na utalii, hii inamanisha hoteli zetu na utalii kwa ujumla. Natamani ingekuwa asilimia kubwa kwa sababu ni kinyume cha matarajio yetu na hili ni kwa sababu ya changamoto ya safari za ndege.” Alisema Nassir
Kwa upande wake Rasmussen, aliyewahi kuhudumu kama Meya na Waziri mkuu nchini Denmark alisema kuwa taifa hilo litaendelea kuimarisha uhusiano wake na taifa la Kenya kiuchumi na kunufaisha mji wa Mombasa huku mataifa haya mawili yakijizatiti kukabiliana changamoto zilizopo.
“Tunataka kuimarisha sekta ya bahari, Denmark ni bora kuliko Kenya,tumekuwa tukishirikiana na mataifa mengine na ndio mana tunahamu ya kusaidia Kenya hasa sekta ya bahari.” Alisema Rasmussen.
Katika kikao hicho Serikali ya Kaunti ya Mombasa ilifanya makubaliano ya kibiashara na serikali ya Denmark ya kuimarisha sekta za kibinafsi na umma.