HabariNews

Afueni kwa Wakenya, Shughuli za kusaka Pasipoti Zikirahisishwa

Huenda wakenya wakapata ahueni katika shughuli za kusaka Pasipoti, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Uhamiaji Evelyn Cheluget alidokeza haya akisema idara hiyo itaboresha mikakati ya utowaji vyeti vya kusafiria.

Cheluget akihutubia maafisa wa uhamiaji katika jumba la Nyayo, alielezea matumaini yake katika shughuli hio akisema itatatua ucheleweshaji wa vyeti hivyo kwa muda mrefu, ambao umezua taharuki kutoka kwa umma.

Kulingana na Cheluget, watumishi katika sekta husika wataongezwa na baadhi ya maafisa kupelekwa nje ya nchi, zamu za mchana na usiku zikitarajiwa kuanza Jumatatu hadi Jumapili huku maombi ya huduma yakipokelewa kuanzia saa 7:00 asubuhi hadi 8:30 jioni.

Miongoni mwa Tiba ya mikakati hio ni pamoja na kukarabati na kununua mashine mpya ambazo zitaruhusu uchapishaji wa pasipoti saa 24/7.

“Tunafanya kazi kwa bidii, sehemu ya pasipoti imekuwa ikifanya kazi kwa zamu, tumeweka kaunta maalum kwa ajili ya kesi za dharura na wakuu wote wa mikoa ili kuongeza wafanyikazi katika kaunta za dharura,” alisema Chegulet.

Wakenya wamekuwa wakihoji ni kwa nini Idara ya Uhamiaji inachukua mda kushughulikia hati hizo za kusafiria, mchakato unaopaswa kuchukua siku 10 hadi 15.

Agosti 24,2023 Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alitoa onyo kwa idara hiyo, akiahidi kulisafisha jumba la Nyayo House.

Mbele ya kamati ya Bunge Alhamisi, Kindiki alihusisha ucheleweshaji vyeti hivyo na ufisadi akiahidi kutapata suluhu ya maradhi hayo.

“Nitasafisha Nyayo House mara moja na kwa wote. Tutaifunga Nyayo House na kuiita eneo la uhalifu. itakuaje Zakenya kupanga foleni kuanzia saa kumi na mbili asubuhi? Haitakuwa kama kawaida. Lazima tuisafishe nyumba ya Nyayo, “ alisema Kindiki.

Aidha Kindiki alifichua mipango ya kupunguza siku za utoaji pasipoti kutoka siku 7 hadi 3 na hata saa 24 kwa matukio ya dharura.

Hata hivyo Kurugenzi ya Huduma za Uhamiaji Ijumaa ilijitetea, ikibaini kuwa katika kipindi cha Julai 13 na Agosti 2023, Jumba la Nyayo lilichapisha vyeti 96,310.