Muungano wa madaktari nchini KMPDU eneo la Pwani sasa unataka huduma za afya kurejeshwa katika mamlaka na usimamizi wa serikali kuu.
Kwenye mazungumzo ya kipekee na Sauti ya Pwani, Katibu wa Muungano huo Ukanda wa Pwani Ghalib Salim, alidai kuwa huduma za afya nchini kupitia serikali za ugatuzi zimekumbwa na changamoto tele na kutaka huduma hizo kurejeshwa katika serikali kuu.
Salim alilalamikia uhaba wa madaktari, kutolipwa kwa mishahara na kutoajiriwa kwa madaktari waliohitimu masomoni kama changamoto zinazolemaza juhudi za utendakazi wao.
“Jambo moja serikali ingefanya, turejesheni kwa usimamizi wa serikali kuu, na iunde mfumo kama vile TSC Tume ya kuajiri walimu madaktari tuwe kwenye usimamizi kama huo. Ushawahi kusikia walimu wakigoma sana, mishahara wanapata kwa wakati, promotion wanapewa wakitaka kwenda likizo wanaenda. Sisi tunapitia changamoto nyingi,” alisema Salim.
Wakati uo huo Katibu huyo aliedokeza kuwa muungano huo utaandaa mgomo iwapoa matakwa na makubaliano yao waliotia sahihi na serikali hayatatiliwa maanani.
“Kama serikali haitashughlikia matakwa na makubaliano yetu tuliyoweka saini na mahakama ikakubali, basi tutagoma tusitishe huduma zetu. Tukigoma si suala la mshahara peke yake hilo lieleweke, hali ni mbaya daktari mmoja anahudumia wagonjwa 200, kuajiri madaktari hawataki, mishahara inacheleweshwa mnataka tufanyeje?” Alisema Salim.
Salim aidha alisema kwamba mgomo huo utakuwa umeambatana na sheria baada ya wao kushtaki mahakamani mnamo 2020 kutokana na kutotimizwa kwa vipengele vya makubaliano ya mazungumzo ya pamoja ikiwemo ahadi ya kuwalipa mishahara yao ya mwaka 2017 mpaka 2021 na ya kuajiri madaktari 4000.
NA MJOMBA RASHID