HabariNews

Shangwe ya Siku ya Makazi Duniani , Wakazi 1000 wapata hatimiliki za ardhi Mombasa

Ni Afueni kwa zaidi ya wakazi 1000 kutoka wadi ya Mikindani eneobunge la Jomvu baada ya kaunti ya Mombasa kuwapa hatimiliki za ardhi wanazoishi.

Kwenye hafla ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya makazi Duniani Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir aliwahakikishia wakazi wa eneo hilo na maeneo mengine ya kaunti kwamba katika uongozi wake hakuna bwenyenye yeyote atakayewahangaisha kutoka kwa makaazi yao.

“Maagizo yangu kwa idara ya ardhi mmesikia kilio cha wakazi. Watu wale ambao wako na ardhi kwa karatasi lazima tuheshimu na wale wakazi wako katika ardhi ambao ni wenyeji pale,” alisema Gavana.

Kwa upande wa walionufaika na ugawaji wa hati miliki hizo wakiongozwa na Philip Mweri Baya walieleza furaha yao baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka 20 kupata vyeti rasmi vya kumiliki ardhi wanazokalia.

“Wee! Si ni raha sana hiyo, maanake zamani hata ile ndoto ya kuwa title deed ilikuwa haiku. Tulianza tuseme mwaka 2000 hadi sasa. Ila ni watu waelemishwe tukilipia ardhi na nyumba tuzipate. Ila kwa leo tuna furaha sana,” alisema mzee Baya.

Haya yanajiri Kenya ikiadhmisha Siku ya Makazi Duniani, huku kaunti ya Mombasa ikilenga kuwafaidi wakazi wake maskwota kwa kuwapa hatimiliki za ardhi sawia na ujenzi wa nyumba za makazi nafuu.

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa Oktoba 2 kila mwaka, kauli mbiu ya mwaka huu 2023 ikiwa ni ‘Uchumi Imara wa Miji: Miji kama vichochezi vya ukuaji na uimarishaji wa miji.’

BY MJOMBA RASHID