Ipo haja ya kudhibiti taasisi za kidini na kuwapiga msasa viongozi wa kidini ili kuhakikishia usalama waumini wao.
Akizungumza na wanahabari Jumanne Oktoba 3 katika maandalizi ya Tamasha la Dini eneo la VOK kaunti ya Mombasa, Mwenyekiti wa Ushirika wa Wachungaji Mombasa, Askofu Zacharia Mwagandi alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuwatambua wahubiri wasiofaa na wenye kuendeleza imani potofu kwa waumini wao ili kuzuia matukio kama ya Shakahola kujirudia.
Askofu Mwagandi aliitaka serikali kushirikiane na viongozi wa makanisa katika kudhibiti makanisa ili kuhakikisha kuwa mwafaka unapatikana na kuchuja itikadi potofu za kidini.
“Serikali kulidhibiti kanisa ni vyema ila kuwe na ushirikiano mkubwa baina ya viongozi wa serikali na viongozi wa makanisa pia, kwa hiyo suala hilo twaliunga mkono,”alisema.
Vile vile Askofu huyo alisema kuwa suala la wahubiri na maimamu kupata mafunzo ya kidini, litawasaidia katika kuwaongoza vyema wafuasi wao kwa misingi inayofaa.
“Tunaunga mkono serikali, ni vizuri wahubiri tujulikane kazi tunazofanya, kisomo changu kimefikia wapi na serikali iwe na mfumo kuangalia wahubiri walio na moyo safi,” alisema askofu Mwagandi.
Kwa upande wake Muevanjilisti Johannes Amritzer alieleza kusikitishwa kwake na matukio ya Shakahola yaliopelekea mamia watu kupoteza maisha kufuatia mafunzo potofu kutoka kwa mhubiri tata Paul Mackenzie, akiwasihi wananchi kuondoa dhana mbaya na kuwataka kutowajumuisha wahubiri wote katika dau sawia.
“Ni janga kubwa sana Kenya na kimataifa limetugusa na tunasikitika kwa hilo kutokea mchungaji unawaambia wafuasi wako wafunge hadi kufa kuonanan na Yesu Kristo. Lakini hata hivyo huwezi kujumuisha kuhukumu watu bilioni 2 kote duniani kuwa potofu kwa maovu ya mtu mmoja huko Shakahola ama mtu anayebadili maandiko ya dini kwa ubinafsi wake.” Alisema Ambritzer.
Wakati uo huo Ambritzer aliwataka waumini wa dini ya kikirsto kujitokeza kwa wingi kujumuika kwenye tamasha hilo la dini kuasherehekea na kujifunza mengi.
Maandalizi ya Tamasha hilo lijulikanalo kama ‘Mlipuko wa Furaha’ , yalikamilika huku tamasha hilo likianza rasmi Jumatano Oktoba 4 hadi siku ya Jumapili Oktoba 8, katika uwanja wa VOK mjini Mombasa.
BY MJOMBA RASHID/BEBI SHEMAWIA