Vijana wanaosaka kazi kwenye meli mjini Malindi, kaunti ya Kilifi wanakabiliwa na hatari ya kutemwa nje ya nafasi za kazi kwa kukosa ufahamu wa lugha ya Kiingereza.
Imebainika kuwa ukosefu wa kujua lugha ya Kimombo ambayo ni kigezo kikuu na lugha muhimu katika sekta ya ubaharia, kumesababisha baadhi yao kukosa nafasi hizo.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa kitengo cha Ajira melini mjini humo Joseph Simbiro hali hiyo imewasababishia vijana wengi kutoajiriwa kwenye nafasi mbalimbali kwenye meli hizo.
“Tulipokuwa katika mahojiano mmoja aliyekuja kama mpishi aliposalimiwa kwa Kizungu akajibu na baada ya hapo akawa bubu hajui aseme nini,sSasa kijana yule alipoteza kazi kwa sababu tu ya kushindwa kuwasiliana kwa kiingereza,” alisema Simbiro.
Afisa huyo akiweka wazi kuwa imelazimu baadhi ya vijana wengine kuhojiwa kwa lugha ya nyumbani angalau wanufaike na mradi huo.
“Wengine ilibidi wafanyiwe interview kwa Kigiriama, na lugha zao za nyumbani sasa mtu unaenda kufanya kazi kwenye meli na pale lugha ya kinyumbani ni wewe peke yako unaijua wengine wote ni kizungu, hiyo itakuwaje sasa?” Alisema
Simbiro aidha amewarai vijana wengi zaidi kujitokeza kutuma maombi ya ajira melini wakati huu ambapo kampuni kadhaa za meli zimetangaza nafasi za ajira.
“Kuna barua tumepata na safari hii wameongeza ajira, kumetokea nafasi za kazi nyingi, kama uuguzi, plumbing, walinzi binafsi, useremala na nyingine nyingi, kwa hiyo wewe kijana ukiwa utatoka mapema kuja kutafuta hizi ajira utakuwa katika nafasi bora. Vijana wasikae tu nyumbani,” alisema.
NA JOSEPH YERI