Kamati ya seneti inayochunguza mauaji ya halaiki ya Shakahola kaunti ya Kilifi imepuuzilia mbali madai ya kuwepo kwa makafani na makaburi katika kanisa la New Life Prayer Centre linalomilikiwa na Mhubiri Ezekiel Odero.
Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake Seneta wa Tana River, Danson Buya Mungatana imetembelea kanisa hilo eneo la Mavueni kubaini iwapo madai yaliyoibuliwa ni ya kweli baada ya Ezekiel kuhusishwa na mhubiri tata Paul Makenzie.
Mungatana anayeongoza kamati hiyo ya wanachama 11 amesema watakutana na Idara ya upelelezi DCI kabla ya kuandaa ripoti yao watakayoiwasilisha bungeni.
“Tumekuja kutafuta ukweli, tuliambiwa kuna mochari na makaburi na tulitaka kujua uhusiano wake huyu tunayemshuku na Makenzie ni namna gani. Lakini tumeona hapa hata kuna mkahawa ndani hata mambo ya kuwa watu waliambiwa wafunge hadi wafe hayapo hapa. Sisi tunaandika vile tumeona yeye si mshukiwa hapa, kama yetu tunachukua ushahidi,” alisema Mungatana.
Kwa upande Mhubiri wa Kanisa hilo lililoko eneo la Mavueni, Ezekiel Odero maarufu Pasta Ezekiel, alishutumu serikali kutaja jina lake kwa Sakata ya mauaji ya shakahola huku akiiomba serikali kufanya uchunguzi zaidi ili kuwakabili wahubiri walaghai.
Odero aliipongeza Bunge la seneti kwa kutikia ualishi wake wa kufika katika kanisa lake hilo kubaini ukweli kabla ya uamuzi kuafikiwa.
“Kamati iliyoteuliwa na serikali inaweza ikafika huku kujua ukweli ulio hapa ndani, Ili tujue uamuzi utakaotolewa iwe uamuzi waliokuja kuona, tunashukuru wamefika tulialika seneti ije ione ijue na kuthibitisha ilichosikia kwa kuona wenyewe,” alisema Pasta Ezekiel.
Ikumbukwe kuwa mnamo Siku ya Ijumaa Oktoba 13, Mhubiri huyo kufika mbele ya Bunge la Seneti kueleza madai ya kuhusishwa kwake na mauaji hayo madai aliyoyapinga vikali.
Odero aliweka bayana jinsi alivyojizoelea umaarufu n ahata chanzo cha fedha za kanisa lake, akisema kuwa zinatokana na sadaka ya ‘fungu la kumi’ zinazotolewa na waumini wa kanisa lake.
Mchungaji huyo alikana ushirika wake na mhubiri tata Paul Mackenzie aliye kizuizini akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya halaiki ya watu zaidi ya 429, pamoja na mashtaka mengine zaidi ya 10.
BY MJOMBA RASHID