HabariNews

Ruto Alilia Uchina kuwekeza Nchini Kenya

Rais William Ruto amehimiza taifa la Uchina kuwekeza zaidi nchini Kenya.

Akizungumza alipozuru kampuni ya China Engineering Corporation Limited inayojishughulisha na suluhu za ujumuishaji wa nishati, ujenzi na ukandarasi, Rais alisema kuwa Kenya itaunga mkono wawekezaji wa kigeni ambao wanaweza kushiriki na kuongezaji thamani inayotumika kwa malighafi nyingi nchi.

Tuna fursa nyingi sana katika nchini yetu ambayo mnaweza kuwekeza huko hasa katika nyanja za Kawi, Maji na makazi,” alisema Rais Ruto.

Katika ziara hiyo jijini Beijing Uchina, Rais Ruto alishuhudia shughuli ya kutia sahihi Mkataba wa Makubaliano kati ya Wizara ya kawi na Mafuta ya Kenya na Wizara ya Kawi ya China.

Wakati huo huo Kenya ilitia saini Makubaliano na kampuni ya mawasiliano ya Huawei ili kukuza mageuzi ya kidijitali. Makubaliano hayo yalitiwa saini na Katibu Mkuu wa Idara ya Kitaifa ya ICT na Uchumi wa Kidijitali nchini Kenya John Tanui, Katibu wa Mambo ya Nje Korir Sing’oei na Gao Fei, Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei Kenya.

Rais Ruto alishikilia kuwa ushirikiano wa Kenya na Huawei utaendeleza miundombinu ya teknolojia ya habari na mawasiliano na kuendeleza uwekaji wa kidigitali katika sekta muhimu kama vile uchukuzi, huduma za serikali mtandaoni, elimu pamoja na afya.

Teknolojia imetuwezesha kuhamisha huduma 13,000 za Serikali hadi kwenye jukwaa la Kidijitali la Huawei na Safaricom miongoni mwa mashirika mengine,” alisema Rais Ruto.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Huawei, Dkt Liang Hua alisema Huawei iko tayari kufanya kazi kwa karibu zaidi na serikali ya Kenya ili kukuza uchumi wa kidijitali na ubunifu nchini humo.

BY EDITORIAL DESK