HabariNews

Kaunti ya Mombasa kuajiri walimu 100 wa Chekechea

Serikali ya kaunti ya Mombasa inapania kuajiri takriban walimu 100 zaidi wa shule za chekechea.

Waziri wa Elimu kaunti ya Mombasa Dkt. Mbwarali Kame alisema hatua hiyo ni njia mojawapo ya kukabiliana na uhaba wa walimu kaunti ya Mombasa.

Kulingana na Mbwarali idadi kubwa ya wanafunzi imekumbwa na changamoto ya walimu jambo ambalo serikali ya kaunti inapania kutatua mipango sawia na kuendeleza ujenzi wa madarasa zaidi mwaka huu.

Mbwarali alisema kuwa hatua hiyo itategemea mgao utakaotolewa kwa serikali ya kaunti.

Kuna upungufu sana, wanafunzi ni wengi walimu ni wachache, tumejadiliana na gavana mwenye na mwaka huu tunanuia kwa uchache walimu 100 shule za chekechea peke yake,” alisema Bw. Kame.

Vile vile waziri huyo alidokeza mikakati ya kuboresha mpango wa lishe shuleni kwa manufaa ya masomo ya wanafunzi akisema kuwa mpango huo utaongezwa kutoka shule za chekechea hadi kwa viwango vya Gredi ya 1 na ya 2 huku ukilenga kunufaisha shule za Kijamii za mitaa ya mabanda.

 

 “Tumefikia kuongeza sisi Mombasa County mambo ya chakula kutoka chekechea ifikie gredi ya kwanza na ya pili na pia kwa shule za mitaa ya mabanda,” alisema.

Tayari kaunti imetenga majiko matatu kwa shughuli za utayarishaji wa lishe inayotarajiwa kupiga jeki wanafunzi sawia na kuimarisha viwango vya elimu.

BY EDITORIAL DESK