HabariNews

JOTO la Nauli! KRC Yatanganza Kupandisha Nauli ya Treni

SHIRIKA la Reli Nchini (KRC) limeongeza nauli ya huduma zote za treni. Hatua hii inajiri baada ya gharama ya bei ya mafuta kupanda maradufu na kutatiza shughuli zake.

Shirika hilo Novemba 1, 2023, lilitangaza nyongeza ya nauli kwa treni ya kisasa inayobeba  abiria maarufu Madaraka Express ya kutoka Nairobi hadi Mombasa, Kisumu Safari Train, Madaraka Express inayohudumu Nairobi na maeneo ya karibu pamoja na Nanyuki Safari Train.

Kulingana na taarifa ya Shirika hilo, abiria wanaotumia treni ya hadhi ya ‘First Class’ kutoka Nairobi hadi Mombasa watalipia Sh4,500 kutoka nauli ya sasa ya Sh3,000, hii ikiwa ni nyongeza ya Sh1,500.

Wasafiri wanaotumia treni ya ‘Economy Class’ kutoka Nairobi hadi Mombasa watalipa Sh500 zaidi, ikiwalazimu kulipia Sh1,500 baada ya nyongeza kutoka nauli ya sasa ya Sh1,000.

Nyongeza hii ya nauli imechangiwa na mabadiliko katika sekta ya kawi na petroli ambapo bei ya mafuta imepanda kwa kiwango kikubwa hali ambayo imeongeza gharama ya huduma zetu zote,” KRC ilisema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Shirika hilo aidha, litawatoza nusu ya kiwango kamili cha nauli watoto wenye umri wa miaka kati ya mitatu na 11 huku watoto wenye umri wa miaka 11 kwenda juu wakilazimika kulipa nauli kamili.

Lakini watoto wenye umri wa chini ya miaka mitatu hawatatozwa nauli yoyote,” KRC ilisema.

Nyongeza hiyo hata hivyo itaanza kutekelezwa Januari 1, 2024, kulingana na KRC, jambo litakalotoa afueni kwa wasafiri nyakati za likizo hasa za msimu huu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

BY EDITORIAL DESK