HabariNews

Kenya na Romania zaitia Saini Makubaliano ya Ushirikiano wa Kibiashara  

Rais William Ruto na Rais wa Romanian Klaus Werner Iohannis wametia saini mikataba minne ya ushirikiano.

Kwenye mikataba hiyo mataifa hayo mawili yaliahidi katika utunzaji wa mazingira na kukabili mabadiliko ya hali ya anga, kufanikisha tafiti mbali mbali mbali kwenye sekta ya kilimo, kudumisha usafi na usalama wa chakula.

Rais alisema Kenya na Romania zinachunguza mikakati ya kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.

 Akiwa katika Ikulu ya Nairobi mnamo Jumanne, rais alisema Kenya ina nia ya kuboresha uwiano wa kibiashara na Romania na kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni.

Majadiliano yetu yalilenga mikakati na afua ambazo kwazo tunaweza kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu,” alisema.

Ruto vile vile alisema amefanya mazungumzo na rais Klaus kuunga mkono juhudi zake za kufanikisha mikakati ya kukabili mabadiliko ya hali ya anga.

Kwa upande wake rais Iohannis alitoa hakikisho la kufanya kazi na Kenya ili kuinua uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Alisema uthabiti wa Kenya unaifanya kuwa kivutio bora cha uwekezaji na lango kamili la Afrika.

 “Kenya ni lango la Afrika, Kenya ni nchi ya kidemokrasia na tulivu yenye matarajio mazuri sana,” alisema Rais Iohannis.

Wakati huo huo rais Ruto alisema Kenya inaendeleza ushirikiano na Romania katika teknolojia ili kuendeleza Silicon Savannah.

Teknolojia inazidi kuwa kiwezesha katika nyanja zote za uchumi, inatupasa kugawana ujuzi na utaalamu,” aliongeza.

Rais Ruto alitoa wito wa kutatuliwa kwa amani kwa vita vya Urusi na Ukraine akisema vimesababisha changamoto kubwa za kiuchumi barani Afrika.

 “Vita vya Ukraine vimeleta hali mbaya barani Afrika, bei za bidhaa kama vile mbolea na nafaka zimepanda,” alisema.

BY NEWSDESK