HabariLifestyleNews

Hali ya Uchumi ni mbaya sana! Utafiti wa TIFA wabaini kilio cha Wakenya

Asilimia 84 ya wakenya wanaamini kuwa hali ya Uchumi ni mbaya zaidi kwa sasa ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Haya ni kulingana na utafiti wa hivi punde uliofanywa na shirika la utafiti la TIFA.

Kwa mujibu wa utafiti huo asilimia 87 ya wakenya imelazimika kupunguza gharama yao ya matumizi kutokana na changamoto ya gharama ya juu ya maisha.

Utafiti huo huo uliofanywa kati ya tarehe 25 Novemba hadi tarehe 7 Disemba kupitia njia ya simu na kuhusisha watu takriban 3,009 umebaini kuwa hali ilikuwa tofauti kipindi sawia na hiki mwaka jana.

Aidha asilimia 39 ya wakenya imetaja mfumko wa bei ya bidhaa za msingi na hali ngumu ya maisha kuwa tatizo kubwa huku asilimia 15 wakitaja ufisadi na asilimia 8 wakitaja malipo ya madeni ya taifa miongoni mwa matatizo mengine yanayokumba taifa hili.

Utafiti huu uliotolewa Jumatano Desemba 13, hata hivyo unaonekana kukinzana na kauli ya rais Ruto, ambaye mnamo Disemba 12, kwneye maadhimisho ya Sherehe za Jamhuri, alibaini kuwa serikali yake imepiga hatua kuimarisha Uchumi katika kipindi cha miezi 6 ikilinganishwa na hapo awali.

“Tumelazimika kutoa mchango wetu katika mapambano ya uhuru wa kiuchumi wa taifa.  Tumelazimika kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi na kuahirisha utekelezaji wa programu muhimu za maendeleo ili kuleta utulivu wa uchumi wetu,”

“Mfumko wa bei sasa umefikia asilimia 6.8 chini kutoka kiwango cha juu cha asilimia 9.2 mwaka jana,” alisema Rais.

Wakati huo huo ripoti hiyo imemtaja waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi kama waziri aliyesafiri zaidi kwenda ng’ambo kwa safari 16 mpaka sasa akifuatwa na mwenziwe wa michezo Ababu Namwamba kwa safari 13.

Aidha waziri wa mwasiliano Eliud Owalo na mwenziwe wa madini na uchumi wa baharini Salim Mvurya walisafiri mara 12 huku waziri wa kilimo Mithika Linturu akisafiri mara 9.

Waziri wa mazingira na mabaliko ya tabianchi Soipan Tuya amesafiri mara 7, naye waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen akisafiri mara 6 huku waziri wa afya Susan Nakhumicha akisafiri mara 3.

Waziri wa masuala ya kitaifa na usalama wa Ndani Prof. Kithure Kindiki na mwenziwe wa elimu Ezekiel Machogu wameripotiwa kutofanya safari hata moja kwenda ng’ambo.

Waziri Kindiki alitajwa kuwa mchapa kazi zaidi na mwenzake wa Kawi Davis Chirchir akitajwa kuwa Waziri aliyefanya vibaya zaidi.

BY MJOMBA RASHID