HabariLifestyleMombasaNews

DCI yasitisha uchunguzi wa madai ya uchochezi dhidi ya viongozi 4 wa Lamu

Idara ya Upelelezi wa jinai, DCI Mombasa imesitisha uchunguzi kuhusu madai ya semi za uchochezi dhidi ya viongozi wanne wa Jamii ya Wabajuni kutoka kaunti ya Lamu waliofika katika makao makuu ya DCI Mombasa Kuandikisha taarifa mapema leo.

Kando na kusitishwa kwa uchunguzi wa wazee hao, viongozi wa kaunti ya Lamu mnamo Alhamisi walikemea hatua hiyo ya kuhangaishwa kwa wazee hao huku wakiapa kusimama kidete kutetea maslahi ya jamii hiyo.

Wakili anayewakilisha viongozi hao Yusuf Abubakar aliitaka serikali kuwa makini katika mipangilio yake ili kuepuka mikanganyiko kama hiyo katika siku za usoni.

Kadhalika ameikosoa serikali kwa kile alichotaja kama kuwasumbua wazee hao ambao wamelazimika kusafiri kutoka kaunti ya Lamu hadi Mombasa ili kuandikisha taarifa yao.

“Ile mikutanao imesitishwa na hakuna wazee kuenda polisi ama mahali popote kujieleza kwa hivyo tunashukuru nkwa yote yaliyotendeka, huu ni usumbufu ambao wamefanyiwa na tunaomba serikali iweze kuwalinda hawa wazee wetu.” Alisema

Akijumuika kutetea wazee hao wanne wa Bajuni, Shakila Abdalla ambaye ni Seneta Mteule wa kaunti ya Lamu alisema wazee hao hawakuwa na makosa na kauli walizotoa za kujipanga hazina uhsama wowote huku akisisitiza kuwa wataendelea kujipanga ili kutetea maswala ya jamii hiyo.

“Wazee hawa hawana hatia, hawakosea mtu, hawajafanya makosa yoyote, wanaambiwa mara waripoti Lamu na DCI mara Mombasa ,kudhalilishwa tu kupotezewa wakati, wazee makosa yao waliyofanya ni kusema wanajipanga na mimi nataka kusema hivi tunaendelea kujipanga hatutarudi nyuma.” Aliongeza Shakila

Kwa upande wake Hassan Abdallah Albeity mmoja wa viongozi kutoka kuanti hiyo aliedokeza kuwa hadi kufikia sasa jamii ya wabajuni inabaguliwa katika maswala ya kupata vitambulisho licha ya kuwa na haki kama Wakenya wengine sasa akitaka serikali kuchukua hatua.

“Kenya kuna haki mahali popote mtu anaeza kuishi lakini vitambulisho hakuna haki ya kwamba sisi tupate kama wengine kwa nini ardhi yetu ya Lamu mtu yeyote anaweza kuishi lakini ikija kwa vitambulisho tuwe sisi lazima tutoe vitambulisho zaidi kwa hivyo tayari serikali yatubagua na hii mazungumzo ya kuwa Kenya Kwanza inalenga Wakikuyu ni kauli ya uchochezi na lazima serikali ichukue hatua.” Alisema Hassan

Idara ya upelelezi, DCI iliwaagiza wanne hao ambao ni Omar Sharif, Mohammed Mbwana, Feswal Mohammed na Abubakar Ahmed kuandikisha taarifa katika makao ya DCI Lamu kwa madai ya kutoa tamko la chuki na Uchochezi katika kaunti hiyo, kabla ya kubadilishiwa na kutakiwa kufika makao makuu ya Idara hiyo mjini Mombasa.

BY EDITORIAL